Madereva Tanga walia kukosa ajira kwenye miradi ya maendeleo

Tanga. Wanachama wa Chama cha Madereva wa Malori Mkoa wa Tanga (Chamata) wamelalamikia ukosefu wa ajira kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa mkoani humo, huku wenzao kutoka maeneo mengine wakipata nafasi hizo.

Madereva hao wametoa malalamiko yao katika mkutano wa ufunguzi wa sherehe za kumbukumbu ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika leo, Januari 29, 2025, katika viwanja vya Community Center, Mtaa wa Makorora, jijini Tanga. Wameiomba CCM kuingilia kati suala hilo.

Mwenyekiti wa Chamata, Abdallah Said, amesema alihamasisha wenzake kuunda chama hicho ili wapate fursa za ajira kwa pamoja, lakini mpaka sasa hawajui nini kinaendelea.

Amesema licha ya wanachama wao zaidi ya 400 kuwa na sifa stahiki na kushiriki usaili wa kazi, majina yao hayarudi kila wanapofanyiwa usaili, bali nafasi hizo hupatiwa wageni.

“Hatujapinga watu kutoka maeneo mengine kupata ajira, lakini tunajiuliza kwa nini sisi wa hapa hatupati? Tunaomba uongozi wa CCM Mkoa wa Tanga ufuatilie changamoto hii na kutafuta suluhisho,” amesema Abdallah.

Amebainisha kuwa miradi mikubwa kama ule wa bomba la mafuta Chongoleani, ujenzi wa barabara ya Tanga-Pangani na miradi ya bandari haijatoa ajira kwa madereva wa Tanga licha ya wao kushiriki usaili mara kadhaa.

Mmoja wa madereva hao, Mambea Pasua, amependekeza kuwa pamoja na kuajiri madereva kutoka maeneo mengine, ni vema asilimia 30 hadi 40 ya nafasi zitolewe kwa wazawa wa Tanga ili kuhakikisha wanapata fursa sawa.

Pia, ameiomba Serikali na viongozi wa chama kufuatilia suala hilo ili madereva wa ndani wapate hata kazi za muda mfupi kama vile kuendesha magari ya kubeba taka.

Akijibu malalamiko hayo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdallah, ameielekeza Serikali ya mkoa kushughulikia suala hilo ili kuhakikisha madereva wa Tanga wanapata ajira kwenye miradi ya maendeleo.

Amesisitiza kuwa CCM haizuii Watanzania kutoka sehemu nyingine kutafuta ajira mkoani humo, lakini ni muhimu kuweka utaratibu wa kutoa kipaumbele kwa madereva wa ndani.

“Tangu waanzishe chama chao, hawajapata fursa hizi, badala yake nafasi zinakwenda kwa watu wa maeneo mengine. Natoa maelekezo kwa serikali kuhakikisha tatizo hili linatatuliwa haraka kwa manufaa ya madereva wetu,” amesema Rajabu.

Ameonya kuwa iwapo madereva hao hawatapata ajira, wanaweza kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu. Hivyo, suala hilo linapaswa kushughulikiwa kwa haraka.

Sherehe za kumbukumbu ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa CCM zimezinduliwa rasmi mkoani Tanga, huku kilele cha maadhimisho kikitarajiwa kufanyika Februari 5, 2025.

Katika hafla hiyo, CCM imewapongeza Rais Samia Suluhu Hassan, Dk Hussein Mwinyi na Dk Emmanuel Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa wagombea wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Related Posts