Marekani Yaitaka Rwanda Kujiondoa Goma – Global Publishers



 

Rais wa Rwanda Paul Kagame

 

Marekani imelitolewa wito Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za kusitisha mashambulizi ya wanajeshi wa Rwanda na waasi wa M23 huko Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana Jumanne jioni ili kuujadili mzozo huu wa Kongo ambapo Kaimu Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Dorothy Shea ametoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano huko Goma na kuitaka Rwanda kuondoa wanajeshi wake nchini Kongo na kurejea mara moja kwenye meza ya mazungumzo ili kufikia suluhu endelevu la amani.

 

Kaimu Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Dorothy Shea

 

Shea amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wajumbe 15, kuchukua hatua za kukomesha mashambulizi ya wanajeshi wa Rwanda na waasi wa M23 lakini hakueleza hata hivyo ni hatua gani zinazoweza kuchukuliwa.

Akihudhuria pia mkutano wa Baraza hilo la Usalama mjini New York, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo Therese Kayikwamba Wagner ameielezea hali ya mashariki mwa nchi yake: “Mamilioni ya watu wameyakimbia makazi yao. Maelfu wamenasa katika mji uliozingirwa wa Goma huku kukiwa na vikwazo vya upatikanaji wa chakula, maji, umeme na usalama. Maisha ya wengi yamepotea. Inatosha. Rwanda haiwezi kuruhusiwa kuendelea na vitendo hivi bila kuadhibiwa. Natoa wito kwa baraza hili kuchukua hatua ili kutetea kanuni na sheria za kimataifa.”

Bi Kayikwamba amelitaka pia Baraza hilo kuwawekea vikwazo viongozi wa kisiasa na kijeshi wa Rwanda, kuwepo vikwazo vya silaha na kupiga marufuku ununuzi wa maliasili za Rwanda na kuwazuia wanajeshi wa nchi hiyo kujiunga kwenye misheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.

Mbali na mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na rais wa Rwanda Paul Kagame na kuendeleza shinikizo kwa serikali ya mjini Kigali na kusisitiza kuwa Washington imesikitishwa mno na kuongezeka kwa mzozo unaoendelea mashariki mwa DRC, hasa kutekwa kwa mji wa Goma na kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda. Baadaye, Rais Kagame amesema ameafikiana na serikali ya Marekani juu ya haja ya kusitisha mapigano mashariki mwa Kongo lakini hakukuwa na dalili zozote kuwa atatii miito inayomtaka kuwaondoa wanajeshi wa Rwanda na waasi wa M23 katika mji wanaoudhibiti wa Goma.


Related Posts