Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, ameondoa marekebisho ya Sheria ya Uhamiaji, Sura 54, katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 4 wa Mwaka 2024, uliolenga kutoa utaratibu wa hadhi maalumu (Diaspora Tanzanite Card) kwa Watanzania wenye uraia wa nchi nyingine.
Aidha, Dk Tulia aliondoa marekebisho ya Sheria ya Ardhi, Sura 113, katika muswada huo, ambayo ilikuwa ikielezea utaratibu wa upatikanaji wa ardhi kwa watakaopewa hadhi maalumu.
Marekebisho hayo yanaondolewa ikiwa ni mara ya pili kuondolewa bungeni, baada ya kuondolewa na Serikali Septemba 4, 2024, kwa kile kilichoelezwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, kuwa ni kutoa nafasi ya kuendelea kufanyia kazi zaidi hoja hiyo.
Hata hivyo, Novemba 8, 2024, Serikali iliurudisha marekebisho hayo ndani ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 4, Mwaka 2024, ambapo ulipelekwa katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa ajili ya kufanyiwa uchambuzi.
Leo, Jumatano, Januari 29, 2025, kabla ya kuwasilishwa kwa muswada huo kwa mara ya pili bungeni, Dk Tulia alimtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, kutowasilisha bungeni sehemu mbili za marekebisho ya Sheria ya Uhamiaji na ile ya Sheria ya Ardhi.
“Muswada wetu una sehemu tisa, lakini katika sehemu ya tano ya Marekebisho ya Sheria ya Uhamiaji na sehemu ya saba inayohusu Marekebisho ya Sheria ya Ardhi, hizi sehemu mbili bado Bunge linafanyia kazi.
“Lakini sehemu zote nyingine ziko tayari. Kwa hiyo, utawasilisha (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) sehemu zote nyingine isipokuwa hizo mbili,” amesema.
Amesema bado Bunge linafanyia kazi sehemu hizo mbili za muswada huo na litakapokamilisha kazi hiyo, utafanyika kwa utaratibu ambao wamejiwekea.
Baadhi ya marekebisho yaliyo katika muswada huo, uliowasilishwa Novemba 8, 2024, Serikali ilipendekeza marekebisho kwa kuongeza vifungu vya 36A, 36B, 36C, 36D na 36E kwa ajili ya kuweka masharti yanayohusu hadhi maalumu kwa raia wa nchi nyingine ambaye aliwahi kuwa raia wa Tanzania au mwenye asili ya Tanzania.
“Masharti hayo yanakusudiwa kutumika kwa mtu ambaye alikuwa raia wa Jamhuri ya Muungano, isipokuwa kwa wale waliokuwa na uraia wa kuasili, au mtu ambaye mzazi wake mmoja, babu, bibi au mtu yeyote katika kizazi kilichomtangulia ni, au alikuwa, raia wa Jamhuri ya Muungano,” ilieleza ma sehemu ya muswada huo.
Johari amesema kuwa kwa mujibu wa vifungu vipya vinavyopendekezwa, pale ambapo mtu anapewa hadhi maalumu, hadhi hiyo itamwezesha kuingia katika Jamhuri ya Muungano na kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Aidha, amesema kuwa hadhi maalumu itaenda sambamba na kupata Kadi ya Tanzanite Diaspora, ambayo itakuwa ni uthibitisho rasmi kwamba mmiliki wa kadi hiyo ana hadhi maalumu.
Amesema vilevile, masharti mapya yanayopendekezwa yanaainisha masuala kuhusiana na muda wa uhalali, wategemezi, masharti na utaratibu wa kufutwa kwa Kadi ya Tanzanite Diaspora.
Amesema kuwa kifungu cha 45 kinapendekezwa kurekebishwa kwa kuongeza neno “Kadi”. Lengo la marekebisho haya ni kuainisha adhabu kwa makosa yatakayotendwa na wamiliki wa Kadi ya Tanzanite Diaspora, kama ilivyo kwa wamiliki wa visa, vibali, vyeti na hati za kusafiria vinavyotolewa chini ya sheria.
Kwa upande wa Sheria ya Ardhi, Sura ya 113, ambapo kifungu cha 19 kinapendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa lengo la kuweka utaratibu wa matumizi ya ardhi kwa mtu aliyepewa hadhi maalumu chini ya Sheria ya Uhamiaji, Sura ya 54.
Kwa mujibu wa marekebisho yanayopendekezwa, mtu aliyepewa hadhi maalumu atakuwa na haki ya kumiliki ardhi kupitia utaratibu wa hati miliki maalumu itakayotolewa na Kamishna wa Ardhi.
Lengo la marekebisho hayo ni kumwezesha raia wa kigeni mwenye asili ya Tanzania kumiliki au kuondosha miliki ya ardhi aliyoipata kwa njia mbalimbali, ikiwemo urithi au kununua.