Mnajaribu kumdanganya nani? Ndugu zangu Wanademokrasia, baada ya kumaliza uchaguzi wenu wa ndani ya chama, nimeona tambo na chumvi nyingi kuhusu uchaguzi huo.
Nimesikia maneno kama vile; “…hiki ndicho chama cha kidemokrasia katika taifa letu…”; “… tumeweka kipimo cha dhahabu, ambacho hakuna ambaye amewahi kukifikia na hakuna atakayejaribu kukifikia…”; “…chama chetu kimeweka rekodi na historia katika bara la Afrika, hakuna mfano…” na mengine mengi sana.
Uhalisia ni kuwa, hizo zote ni kutia chumvi na ni kujipa moyo tu. Kiuhalisia, ndiyo kwanza mnaianza safari, kwa kadiri ninavyofahamu, kwa kadiri ya uzoefu wangu, mmeweka vichwa ardhini mkiamini mnajificha, lakini punde si punde mtagundua mko hadharani, ni suala la muda!
Ukweli ni kwamba, mmefanya uchaguzi wenu na kumaliza salama na mshindi ametangazwa!
Huu ni utaratibu wa kawaida kabisa wa kidemokrasia na unafanyika kila mahali, kwa hapa Tanzania, CCM imekuwa na utaratibu wa kidemokrasia ndani ya chama, kwa kipindi kirefu sana.
Labda nitoe somo kidogo, kuna tofauti ya namna vyama na taasisi kongwe zinavyoendesha mambo yake ukilinganisha na namna vyama au taasisi changa zinavyoweza kujiendesha.
CCM ni taasisi kongwe, imara, yenye ufanisi, inayonyumbulika na kujinyumbua (flexibility) kila wakati kulingana na nyakati na mahitaji ya nyakati hizo. Taasisi za namna ya CCM hufanya uamuzi wake mapema sana, huona mbali mapema mno, na huchukua hatua mapema sana kwani zinao viraka ambao ni full packages kwa kadiri wakati utakavyojitaji.
Taasisi za namna hii huandaa viongozi katika kipindi kirefu mno, huwalea, huwatunza na huhakikisha viongozi hao wanakuja kuisaidia taasisi na nchi katika nyakati ambazo aina hiyo ya viongozi inahitajika.
Nitoe mfano wa Dk Nchimbi. Ni kiongozi ambaye alipikwa na hakutupwa, ameandaliwa tangu kuongoza UVCCM, kisha akawa Mkuu wa Wilaya, kisha mbunge, Naibu Waziri, Waziri, Balozi, Katibu Mkuu wa chama na sasa ni mteuliwa katika nafasi ya mgombea mwenza kwa ajili ya uchaguzi wa Oktoba 2025 kwa tiketi ya CCM.
Unaweza kuona, aina hii ya watu, akisimama popote, Watanzania wanamfahamu vizuri, wanajua alivyoandaliwa vya kutosha na hawawezi kuwa na shaka na uwezo wake.
Muangalie Dk Samia, mwangalie Dk Mwinyi, waangalie viongozi wengi wa CCM walivyopikwa na kuandaliwa kwa uhakika na kwa muda mrefu.
Michakato ya kidemokrasia
Ukizungumzia demokrasia, tunaangalia michakato ya ndani ya kupata vinara wa uongozi kwa niaba ya wengine, CCM ndiye kinara wa hilo. Unaweza kujiuliza, Hayati Mwalimu Nyerere aliwezaje kung’atuka madarakani kama chama chake kisingekuwa cha kidemokrasia?
Hayati Mzee Mwinyi, aliwezaje kuingia na kuondoka kwenye uongozi wa nchi na uongozi wa chama ndani ya miaka 10? Hayati Mzee Mkapa? Mzee Jakaya? Hayati Mzee JPM? Na hata sasa Dk Samia, nani anaweza kuthubutu kusema hatatoka kwenye nafasi ya uenyekiti wa chama na urais wa nchi baada ya miaka hii mitano, Mungu akituweka hai?
Tumewafuatilia Democrats halisi?
Demokrasia ni nini basi? Rais Biden wa Marekani, nchi ambayo ni baba wa demokrasia, alipoona hataweza kushindana na Rais Donald Trump kwenye mtanange wa urais, chama kikubwa kama Democrat mliona walichofanya?
Hakukuwa na fomu za kugombania tiketi ya urais kupitia Democrat, badala yake Rais Biden alimu-endorse (alimuidhinisha) Makamu wa Rais Kamala Harris kuwa mgombea urais. Mkutano mkuu wa Democrat ulipokutana, hakukuwa na watia nia wa nafasi ya urais ndani ya Democrat, siyo kwamba hakuna watu wenye uwezo, lakini Rais Biden aliamua kuwa watakwenda na Kamala, na DNC ilipokutana hotuba zote zikawa kumuidhinisha Kamala Harris! Mlifuatilia?
Unajua ni kwa nini? Ni kwa sababu vyama vikubwa duniani, imara, vinavyonyumbulika, huwa havisumbuki nyakati za kufanya maamuzi, na havitetereki.
Niliona baadhi ya watoa hoja upande wa pili, wanasema ati “…CCM imekimbia demokrasia kwa kutotoa fomu kwa wanachama ili washindane kupata mgombea urais…”
Wanaosema hivyo; Mosi, hawahoji kuhusu Biden, DNC na Democrat (mababa wa demokrasia duniani).
Pili, hawataki kueleza uhalisia na utamaduni wa CCM, kwamba kila kunapokuwa na Rais madarakani (incumbent) na akawa ametumikia miaka mitano peke yake, miaka mitano ya pili huwa anakuwa “endorsed” ili aendeleze kazi nzuri aliyoianzisha, kwa miaka mingine mitano, kwa sababu akishamaliza hii mitano ya pili, kwa mujibu wa Katiba yetu, mtu huyo hawezi kuwa Rais tena, hata kama angalipendwa sana.
Tatu, hawataki kueleza ukweli kwamba, kila baada ya miaka 10, CCM huingia kwenye “full swing democratic process” ambapo wanachama wanaotaka kugombea nafasi ya urais, huchukua fomu na kushindana na kushindanishwa na kuchakatwa hadi chama kumpata mbeba maono mmoja.
Nne, hawataki kuzungumzia ukweli kuwa, kila baada ya miaka mitano, CCM huingia kwenye uchaguzi wenye ushindani na demokrasia pana, ambapo wanachama huchukua fomu, kushindanishwa kidemokrasia na hatimaye kupata viongozi wa mashina, matawi, kata, majimbo, wilaya, mikoa na taifa. Michakato yote hii ni ya kidemokrasia kwa asilimia 100.
Sasa inashtua na kushangaza sana, kwamba chama kinakutana ukumbini, kinaendesha mapambano makali ya kumuondoa mwenyekiti aliyekaa miaka 21 madarakani, halafu kinafanikiwa na moja kuanza tambo kuwa “…tumeweka a golden standard…(kipimo cha dhahabu)”, hivi ni vituko na vichekesho!
Kipimo kilishawekwa kabla
Yani, wanaotenda na kubadilishana madaraka kwa utulivu na amani kila kukicha, mpaka imekuwa siyo ishu kwao, unaweza kudai wao hawana demokrasia? Halafu nyinyi ambao mkutano mmoja umewatoa jasho mpaka mmechanganyikiwa na mmefanikiwa kumng’oa kiongozi wenu na hadi leo hamuamini kama kweli kang’oka au hayupo, halafu hiyo ndiyo golden standard na eti vyama vingine vije vijifunze kwenu!
Yaani Democrat wa Marekani waje wajifunze kwenu? CCM ya Tanzania ije ijifunze kwenu! Mko serious? How dare would you say that, one successful deed ever in your party is a golden standard to a country like this and in Africa? (Mnawezaje kusema kitendo kimoja cha kwanza cha mafanikio ya kidemokrasia kwenye chama chenu ni kipimo cha dhahabu kwa nchi yetu na Bara la Afrika?
Chama cha ACT Wazalendo, cha kina Zitto Kabwe mathalani, mbona kina rekodi bora zaidi za ukomo wa madaraka na kubadilishana madaraka na kufanya chaguzi za kidemokrasia za ndani ya chama chao kiushindani, toka kimeanzishwa, lakini hatujawahi kusikia kikidai kime-set golden standard?
Kipimo halisi kifichwacho
Honestly Speaking (kuzungumza kwa dhati), kilichowatokea mwaka huu ni kufanikiwa kumng’oa Mwamba! Nothing more nothing less (hakuna kubwa zaidi) mlilofanya! Na baada ya kumng’oa, kwa uzoefu wangu, mtaanza mapambano ya kushughulikiana ndani kwa ndani na haya yatawachukua miaka kadhaa mbele hadi mjitoe kwenye hiyo minyororo!
Ndiyo kwanza nilimsikia Wakili Mwandamizi, Tundu Lissu, mwenyekiti wa sasa, akidai sasa anaanza michakato ya kuweka ukomo wa madaraka pamoja na mambo mengine.
Yani chama kinachodai kimeweka golden standard kwenye demokrasia, wakati huohuo kinasema ndo kinaanza kujenga mifumo yake ya ndani ya kidemokrasia, mnamdanganya nani? Mbona mnajidanganya ninyi wenyewe?
Ni ushauri wangu kwenu, kwamba mnayo kazi kubwa sana ya kufanya kuliko kujiaminisha kuwa kuna mteremko mbele yenu, kupambana na chama kikongwe na kikubwa kama CCM hakuwezi kufanywa kwa vitisho, mbwembwe na tambo bila kuwa na mtandao mkubwa hadi katika ngazi ya kaya kama ilivyo CCM. Kalaghabaho!