Seoul. Majanga katika usafiri wa anga yameendelea kuikumba Korea Kusini baada ya ndege ya Shirika la Busan nchini humo kushika moto muda mfupi kabla ya kuanza safari yake kwenda Hong Kong.
Shirika la Habari la Associated Press (AP) limeripoti kuwa ndege hiyo imeshika moto saa 4:30 usiku wa kuamkia leo, Jumatano, Januari 29, 2025, katika Uwanja wa Kimataifa wa Gimhae nchini Korea Kusini.
Taarifa ya Jeshi la Zimamoto nchini humo imeeleza abiria wote 169 na wahudumu saba wameokolewa, huku watatu wakipata majeraha kutokana na moto huo.
Jeshi hilo pia limesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa moto huo ulianzia kwenye mkia wa ndege hiyo, kisha kusambaa kwenye maeneo mengine. Hata hivyo, baada ya king’ora cha moto kulia, zimamoto walifika kwa wakati na kuudhibiti.
Vipande vya video vinavyosambaa mitandaoni vinaonyesha maofisa wa uokoaji wakiwasili eneo ilipokuwa ndege hiyo, huku wengine wakipambana kuuzima moto huo.
Baadaye, video iliyorushwa na Shirika la Habari la Yonhap imeonyesha matundu ya kuungua kwenye mwili wa ndege hiyo, kuanzia juu hadi uvunguni mwa ndege hiyo ya Shirika la Busan.
Tukio hilo limetokea ikiwa ni mwezi mmoja tangu kutokea kwa ajali mbaya katika historia ya ajali za ndege nchini Korea Kusini, iliyohusisha ndege ya Shirika la Jeju iliyokuwa ikitokea Bangkok, Thailand, kwenda Uwanja wa Muan nchini humo.
Ajali ya ndege ya Shirika la Jeju iligharimu maisha ya watu 179, wakiwemo abiria na wahudumu, huku wahudumu wawili pekee wakinusurika kifo. Hata hivyo, walioathiriwa walipata majeraha makubwa mwilini mwao na wanaendelea na matibabu nchini humo.
Shirika la ndege la Busan ni kampuni tanzu ya Asiana Airlines ya Korea Kusini, ambalo Desemba 2024, lilichukuliwa na kuwekwa chini ya usimamizi wa Shirika la ndege la Korea.
Watengenezaji wa ndege hiyo, Kampuni ya Airbus, wametoa taarifa wakisema wamefahamishwa kuhusu ajali hiyo, huku wakiahidi kufanya ufuatiliaji ili kubaini chanzo.
Hata hivyo, mashirika ya ndege Busan na Asiana, yalipotafutwa na Associated Press kuzungumzia ajali hiyo, hayakutoa kauli yoyote.
Kwa mujibu wa Mtandao wa Usafirishaji wa Anga, ndege iliyowaka moto ni modeli iliyovumbuliwa miaka 17 iliyopita, ya Airbus A321ceo yenye mkia namba HL7763.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika.