Binadamu hujifunza kutokana na makosa, lakini kuna watu walisema: “Ni mjinga tu anayejifunza kutokana na makosa yake.” Walimaanisha kila mtu huyaona mambo kwenye upeo wake tu, hivyo hulazimika kujifunza kutoka kwa wengine ili kuyaona yaliyo nje ya upeo wake. Asiyetaka kujifunza kutoka kwa wengine huyarudia makosa yake pasipo kujua njia za kuyaondoa. Atarekebisha makosa ya zamani kwa makosa mapya, yaani anashona kiraka juu ya kiraka.
Juma lililopita, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilifanya uchaguzi wake mkuu. Kama kawaida ya chaguzi duniani kote, tambo na kejeli zilihanikiza kwenye kampeni. Kulikuwa na kila dalili za uchaguzi kugubikwa na fujo na udanganyifu, ukizingatia ushindani mkubwa kwenye kambi za Freeman Mbowe na Tundu Lissu. Kadhalika kihistoria, Chadema haina uzoefu wa kutosha katika mabadiliko ya uongozi wa juu.
Kama jinsi ambavyo binadamu anajifunza maishani, kadhalika katika siasa kila chama hurekebisha mapungufu yaliyomo kwenye mfumo wake kupitia vyama pinzani. Inawezekana chama kikawa na umri mrefu tangu kuzaliwa, lakini bado kikawa na mapungufu kwenye mifumo. Siyo dhambi kuiga mazuri ya mwendawazimu na kuachana na mabaya ya wenye akili timamu. Kimsingi jambo zuri hubaki hivyo hata likitendwa na kichaa.
Kule Marekani tunashuhudia mabadiliko makubwa ya kisiasa kila wakati. Vyama mahasimu wakuu wamekuwa wakibadilishana ushindi kila mara kutokana na sera zao katika wakati husika. Na kila kambi ndani ya vyama hujifunza mbinu na mikakati kutoka kwa washindani wao.
Mapema tulishuhudia uchaguzi wa serikali za mitaa hapa nchini. Figisu zilitawala kwenye maeneo mengi kabla na wakati wa uchaguzi. Mapema wakati wa teuzi za wagombea zilizofanyika, hasa ndani ya chama tawala zililalamikiwa na wanachama wa chama husika. Kulikuwa na malalamiko ya kulazimishwa kuwabeba wagombea waliokuwa si machaguo ya wapigakura.
Palifikia mahali pa baadhi ya wanachama kutishia kuugomea uchaguzi huo, au kupiga kura za chuki.
Katika hili chama tawala na Serikali hawana cha kujitetea. Matatizo mengine ni aibu hata kuyasema.
Kwenye zoezi kubwa kama uchaguzi, ni jambo la kushangaza “Tume Huru” kukosa mbinu za kupunguza au kuyaondoa kabisa matatizo yaliyolalamikiwa katika chaguzi zilizopita. Haikutegemewa pia tume hiyo kukosa vifaa na wataalamu kiasi cha kubandika majina yasiyosomeka vituoni.
Kwenye baadhi ya vituo, karatasi zilizokuwa na majina ya wapigakura ziliandikwa kwa mkono na bila mpangilio wa alfabeti. Hilo liliwatatiza wapigakura ambao baadhi walifika alfajiri na kutafuta majina yao hadi mchana kabla ya kukata tamaa na kuondoka. Pamoja na hayo, yalionekana majina ya wagonjwa mahututi na marehemu, na ofisi za tume zilifungwa mapema, hivyo kuzuia malalamiko ya wananchi kupokelewa.
Kuengua majina ya wagombea wa upinzani nalo lilikuwa doa lingine. Nilisema wakati ule kuwa mtihani uliokosewa kutungwa unaathiri watahiniwa wote, hivyo marekebisho ya jumla ni lazima yafanyike kwa wote. Haileti picha nzuri ya kurekebisha makosa ya baadhi ya watahiniwa na kuyaacha ya wengine. Kwa vyovyote umma wa Watanzania utaona kuwa hizo ni njama za kudidimiza mawazo mbadala.
Kilichotokea kilikuwa sawa na mama asiye na busara anayemwaga upupu kwenye kitanda cha dada wa kazi. Kitanda hicho kikilaliwa na binti yake kilio kitamrudia mwenyewe. Mwindaji ananasa kwenye mtego wake, na ndicho kilichotokea kwenye uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa.
Kambi ya upinzani ililia, lakini tumeona wahafidhina wa chama tawala wakisikitishwa na mwenendo mzima wa zoezi hilo.
Tumeshuhudia ukomavu wa kidemokrasia kwenye chama hiki cha upinzani. Iwapo chaguzi zetu zingefuata njia za uchaguzi mkuu wa Chadema, Taifa letu lingeendelea mara mia. Na iwapo maneno yaliyotamkwa na viongozi waliokuwa washindani kwenye zoezi hilo yatatimia, Watanzania tutakuwa tumeandika historia muhimu sana ya uchaguzi duniani kote. Wenzetu watakuwa na cha kujifunza kutoka kwetu.
Wakati mwingine makosa hayafanywi na vyama au Serikali moja kwa moja, bali hufanywa na watendaji mmoja mmoja.
Watendaji hawa huwa na woga wa kuachwa kwa sababu za kukosa sifa. Hivyo huamini kuwa wakimpatia ushindi mgombea wao atawaamini na kuwabakiza kundini.
Njia pekee ya kuufikia ushindi batili ni njia za panya, na huo ndio mwanzo wa mazingaombwe na sarakasi kwenye uchaguzi.
Hapa Serikali inaingia lawamani kwa sababu inashindwa kuchukua hatua dhidi ya watendaji wabovu.
Na ni kwa sababu hiyo, haramu hii huonekana halali. Hata watendaji wapya wataamini kuwa figisu ni mkakati wa ushindi baada ya kuona waliowatangulia wakizila mbivu.
Serikali inapaswa kuamini kuwa uchaguzi huru na wa haki haupimwi kwa chama fulani kushinda, bali ni ule usio na malalamiko.
Washindi wafurahie ushindi wao, na washindwa wakubali matokeo na kukaa kwenye nafasi yao ya usaidizi. Ndiyo maana nasisitiza dunia inacho cha kujifunza kutoka kwenye uchaguzi mkuu wa Chadema.
Hongereni sana Watanzania.