Rais Samia ampongeza Padri Mihali kuteuliwa Askofu wa Jimbo la Iringa

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amempongeza Padri Romanus Elamu Mihali kwa kuteuliwa na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Fransisko, kuwa Askofu mteule wa Jimbo Katoliki la Iringa.

Padri Mihali aliteuliwa jana Jumanne, Januari 28, 2025, kuchukua nafasi ya Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, baada ya kuridhia ombi lake la kustaafu.

Leo Jumatano, Januari 29, 2025, Rais Samia ametumia mitandao yake ya kijamii kumpongeza Mihali, ambaye awali alikuwa Makamu wa Askofu kwa Waklero wa Jimbo la Mafinga.

Rais Samia ameandika: “Pongezi za dhati kwa Baba Askofu mteule Romanus Elamu Mihali kwa kuteuliwa na Papa Fransisko kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Iringa. Uteuzi wako ni ishara ya imani kubwa ya kanisa kwa utumishi wako. Nakutakia kila la kheri.

“Mwenyezi Mungu akushike mkono, akubariki na kukuongoza unapoendelea kushiriki kazi yake ya kuijenga jamii yetu kuwa bora zaidi katika jukumu hili jipya.”

Rais Samia amehitimisha ujumbe wake kwa kunukuu maandiko matakatifu kutoka Kutoka 4:12: “Basi sasa, enenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalolinena.”

Related Posts