Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, ameeleza sababu ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kutofika kumkabidhi ofisi mwenyekiti mpya Tundu Lissu, akisema haikuwa lazima.
Lissu, aliyeshinda katika uchaguzi wa chama hicho Januari 22, alifika ofisi za makao makuu Mikocheni, jijini Dar es Salaam leo Jumatano, Januari 29, 2025 saa 5:00 asubuhi, akiambatana na viongozi wenzake, na kulakiwa na Mnyika. Walifanya kikao kifupi kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari.
Akizungumza kuhusu sababu ya Mbowe kutokuwepo kukabidhi ofisi, Mnyika amesema kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho, yeye ndiye msimamizi mkuu wa ofisi.
“Kwa kuwa hakukuwa na mabadiliko ya Katibu Mkuu, mimi ndiye nimewapokea Mwenyekiti na Makamu na viongozi wengine,” alisema Mnyika.
“Kwa Katiba ya Chadema, mwenyekiti sio mtendaji, mtendaji ni Katibu Mkuu, mafaili yote anayo. Hivyo, hata mwenyekiti angekuja ingekuwa tu ni kwa ajili ya kutimiza wajibu wa kisheria,” ameongeza.
Akaongeza, “Hakuna kipindi cha mpito kwa katiba yetu, wala hakuna kuapishwa, hivyo Mbowe alishakabidhi uenyekiti pale Mlimani City.”
Akizungumza na waandishi wa habari, Lissu amesema, “katika hii siku ya kwanza ofisini, kwa mapokezi yenu, nafikiri tumeanza vizuri. Hao wanaosema hawa wabangaizaji wataendeshaje chama, tuwathibitishie kwamba tunaweza.”
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti (Bara), John Heche, amewataka wanachama kutembea kifua mbele.