Rukwa. Serikali inakusudia kununua boti maalumu ya kisasa kwa ajili ya shughuli za uokoaji wa wavuvi katika ukanda wa Ziwa Rukwa, hususan pale dhoruba kali ya upepo inapotokea.
Kauli hiyo imetolewa leo, Jumatano, Januari 29, 2025, na Mbunge wa Kwela ambaye pia ni Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu, baada ya ibada ya misa ya kuwaombea wavuvi tisa waliopoteza maisha kutokana na dhoruba iliyotokea ndani ya Ziwa Rukwa.
Sangu amesema boti hiyo si tu itatumika kwa shughuli za uvuvi, bali pia itakuwa msaada mkubwa katika operesheni za uokoaji endapo maafa yatatokea.
Aidha, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuguswa na tukio hilo na kusaidia kuwaokoa wavuvi 540 waliokuwa wakifanya shughuli za uvuvi Ziwa Rukwa.
“Uamuzi wa Rais Samia Suluhu kuagiza ipelekwe helikopta ya jeshi pamoja na wapiga mbizi wapatao 50 wakiwa na vifaa maalumu vya uokozi unaonyesha jinsi anavyothamini maisha ya wananchi wa Jimbo la Kwela na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla,” amesema Sangu.
Baada ya misa hiyo iliyofanyika katika vijiji vya Ilemba na Nankanga kwa ajili ya kuwaombea wavuvi waliopoteza maisha, Sangu amewataka wananchi kuwa watulivu na kuendelea kuwaombea marehemu.
Amesema vikosi vya uokoaji vilivyotumwa vilitoa msaada mkubwa kwa kushirikiana na wananchi, na kama visingefika kwa haraka, madhara yangekuwa makubwa zaidi.
Katika operesheni hiyo ya uokoaji, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji, na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF), John Masunga, walifika kuungana na wananchi wa Bonde la Ziwa Rukwa kusaidia juhudi za uokoaji.
Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, hadi sasa wavuvi tisa kati ya kumi waliokuwa wakitafutwa tangu Januari 23, 2025, wamepatikana wakiwa wamefariki dunia. Miili minne imetambuliwa na ndugu zao, huku miili mingine mitano ikiwa imezikwa kutokana na hali ilivyokuwa.
Sangu pia amepongeza wananchi kwa kushiriki kikamilifu katika uokoaji na kutoa ushirikiano wa kuwatambua wavuvi wengine ambao hawakuwa wamesajiliwa kwenye vikundi na kampuni rasmi ya uvuvi.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Chirukile, amesema mwili wa mvuvi mmoja aliyefahamika kwa jina la Ngosha bado haujapatikana, huku juhudi za kuutafuta zikiendelea.
Kwa upande wake, mkazi wa Kata ya Ilemba, Agustino Mashaka, ambaye pia ni miongoni mwa manusura wa tukio hilo, amemshukuru Mwenyezi Mungu na Serikali kwa jitihada zilizofanyika kuhakikisha waathirika wanapata msaada.
Maafa hayo yalitokea Januari 23, 2025, majira ya saa tatu asubuhi katika Bonde la Ziwa Rukwa, ambapo wavuvi 550 waliingia ziwani kwa shughuli za uvuvi wa kawaida lakini walikumbwa na dhoruba kubwa.