Arusha. Serikali, kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), imesikia kilio cha wadau wa utalii nchini dhidi ya mabadiliko mapya ya tozo zilizoanza kutumika Januari 17, 2025.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Jumatano, Januari 29, 2025, Kamishna wa Tawa, Mlage Kabange, amesema wamesikia hoja za wadau hao na wanatarajia kukutana nao tena kwa lengo la kujadili suala hilo.
Hata hivyo, Tawa imetoa kauli hiyo baada ya kupita siku mbili tangu wadau wa utalii kuzungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, wakipinga utekelezaji wa mabadiliko mapya ya tozo za kuingiza watalii kwenye mapori yao na kwenye maeneo ya Mapori Tengefu ya Hifadhi ya Jamii (WMA).
“Hakuna kanuni zinazoweza kupitishwa bila ushirikishwaji. Kila jambo tulizungumza, tulijadiliana na tukakubaliana, ndipo zikapitishwa. Lakini kwa sababu wamesema hivyo, tumeagizwa na wizara yetu kurudi mezani na wadau hao ili kujua tatizo lilipo, na mtapata mrejesho,” amesema Kabange.
Awali, wadau wa utalii, wakiwemo Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO), walipinga mabadiliko ya tozo mpya kwenye Mapori Tengefu zilizotangazwa hivi karibuni na Tawa kwa madai kuwa ni kubwa tofauti na uwezo wao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa TATO, Henry Kimambo, amesema tozo hizo zimeongezeka kutoka asilimia 30 hadi kufikia asilimia 650.
Amesema huo ni mzigo mkubwa kwa watalii wengi wanaotarajia kuingia nchini, kwani tayari walishafanya malipo mwaka jana.
“Tumeona tangazo mwaka huu, na tozo hizi zinaanza kufanya kazi mwezi huu, wakati wageni wengi wa msimu huu tunaotarajia kuwapokea walishafanya malipo tangu mwaka jana na wanachosubiri ni ratiba zao.
“Sasa unapoongeza tozo sasa, maana yake kampuni ibebe hasara hiyo, au tuwarudie wageni wetu, kitendo ambacho kitatufanya tuonekane kama matapeli tusio na kauli au msimamo katika bei zetu,” amesema.
Kimambo amesema baadhi ya tozo zinazowakabili na kuwa changamoto kubwa kwao ni pamoja na ada ya madereva wa watalii, ambayo imeongezeka kutoka Sh8,260 hadi Sh41,300.
“Tozo ya gari, ambayo imepanda kutoka Sh17,700 hadi Sh23,600. Tozo ya kiingilio kwa mtalii, kutoka Sh30,149 hadi Sh70,800.
Tozo ya kitanda kwa usiku, kutoka Sh45,223 hadi Sh59,000, huku dereva wake akitakiwa kulipa Sh23,600, kutoka Sh5,900,” amesema.
Akizungumzia mkutano wa makubaliano ya mabadiliko hayo, Kimambo amekiri kuwa walikaa kikao na kutoa mapendekezo ambayo yalihitajika kuchakatwa na kurejeshwa kwao kwa ajili ya kukubaliana ili ziweze kupitishwa.
“Tunashangaa haya mambo kwenda kwa haraka hivyo, wakati bado tulikuwa kwenye mchakato wa kutengeneza na kurudisha ili kukubaliana kiwango na lini zianze kutumika,” amesema.
Amesema madhara ya kung’ang’ania kiwango cha tozo hizo yatapunguza idadi ya wageni na kudhoofisha juhudi za Serikali za kuutangaza utalii.
Pia amesema hatua hiyo itanyima mapato vijiji vinavyonufaika na Mapori Tengefu ya Hifadhi ya Jamii, kwa sababu watalii wengi watashindwa kumudu gharama hizo.