Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania na Burundi zimeingia makubaliano ya kuanza ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Uvinza hadi Musongati nchini Burundi (Km282) huku mradi huo ukitajwa kufungua uchumi katika maeneo makuu manne.
Mradi huo uliogharimu Sh5.38 trilioni unategemewa kutekelezwa kwa miezi 72 (miaka 6) na unatajwa kufungua uchumi katika sekta ya umeme, madini,mawasiliano pamoja na kuchochea biashara baina ya mataifa hayo mawili.
Tayari Kampuni ya China ya CREGC&CREDC imepewa jukumu la kuanza ujenzi wa reli hiyo, kazi itakayoanza wiki mbili baadaye kuanzia sasa.
Akizungumza leo Jumatano, Januari 29,2025 katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa -SGR kutoka Uvinza Tanzania hadi Musongati nchini Burundi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara amesema yapo mataifa mbalimbali yameona fursa ya kujiunga na ujenzi wa SGR.
“Burundi wameingia,DRC wameingia na reli ni fursa kubwa kwasababu inakuza biashara ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), reli hii ni ya kisasa ni zaidi ya kubeba mizigo na abiria inaweza kusafirisha umeme,megawati 300 sio mchezo lakini TRC wanaweza kuzibeba,” amesema.
Kupitia treni hiyo, Profesa Kahyarara amesema nchi ambazo hazina bahari watasafirishiwa huduma za internet akifafanua kuwa mashirika makubwa ya reli duniani yanapata fedha kupitia huduma za mawasiliano.
Mbali na hayo, amesema treni ya SGR inatumia nishati safi hivyo inapunguza utoaji wa hewa ya ukaa na hiyo ni faida kwa Tanzania kutekeleza kwa vitendo agenda ya nishati safi.
Akizungumzia kuhusu umeme, Profesa Kahyarara amesema treni inapokimbia inazalisha umeme kwahiyo TRC pamoja na kutumia umeme inazalisha nishati hiyo kwa asilimia 15 na huingia kwenye gridi.
Kwa eneo la madini, amesema SGR itakapopita eneo la Musongati upo mgodi mkubwa wa madini ya Nickel hivyo wataangalia namna ya kuchukua fursa hiyo.
Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo yake kwa TRC amelitaka shirika hilo kusimamia mradi huo kutekelezwa kulingana na mkataba.
“TRC hakikisheni mnafuata viwango vya usalama vya kimataifa vya utekelezaji wa mradi pia usimamizi wa fedha za mradi kusiwe na gharama zisizo za lazima wananchi wanaostahili fidia walipwe,” amesema.
Mbali na hayo amesisitiza ajira zinazotokana na mradi huo ziwanufaishe wananchi waliopo karibu na miradi pamoja na kutolewe hisani kwa jamii kupitia mradi huo.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Uchukuzi Burundi Dieudonne Dukundane amesema kwa miaka mingi aliyofanya kazi Kenya na Tanzania ameona mafanikio makubwa ya SGR.
“Nimeona jinsi SGR ilivyoanza Kenya nikaona mlivyoanza SGR Tanzania, hayo yote Burundi lilikuwa ni somo, ninaweza kuwahakikishia ya kwamba mfano niliouona Tanzania ni mfano wa kuigwa kwa bara lote la Afrika,” ameeleza.
Amesema ujenzi wa reli hiyo sio tu utakuwa fursa ya kuimarisha uwekezaji baina ya Tanzania na Burundi bali utaimarisha biashara ukanda wa Afrika Mashariki.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TRC Masanja Kadogosa amesema ujenzi wa reli hiyo itahusisha vipande viwili,kipande kutoka Uvinza – Malagarasi na Malagarasi – Musongati.
Kadogosa ameeleza kuwa thamani ya mradi huo wenye urefu wa kilomita 282 ni Sh5.6 trilioni na utekelezaji wake ni miezi 72 na 12 itakuwa ya matazamio.
“Km 240 ni za njia kuu na km 42 ni za njia za kupishania na kupitia mradi huu utajengwa daraja linalounganisha Tanzania na Burundi na stesheni saba na fedha za utekelezaji zinatoka Benki ya Maendeleo Afrika (AFDB),” amesema.
Akisisitiza eneo hilo, Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo Africa AFDB Mumina Wa-kyendo amesema uwekezaji wa SGR ni moja ya miradi mikubwa duniani ambayo kwa Tanzania umeifanya sekta ya usafirishaji pekee kufikia uwekezaji wa dola Sh12.7 trilioni sawa na asilimia 70 ya uwekezaji wa Benki hiyo nchini Tanzania.
Amesema uwekezaji huo ni ushuhuda Serikali imewekwa nia ya kuwekeza katika miundombinu hasa usafirishaji.