MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Al Talaba ya Irak, Simon Msuva amesema bado anaikumbuka Morocco tangu aanze kucheza soka la kulipwa nje msimu bora kwake uliomfungulia milango ni 2017/18 alipoitumikia Difaa El Jadida. Msimu huo Msuva alijiunga na Difaa El Jadid akitokea Yanga ambako alifanya vizuri 2016/17 akimaliza kinara wa mabao 14 sawa na Abrahaman Mussa aliyekuwa Ruvu Shooting.
Akizungumza na Mwanaspoti, Msuva alisema akiwa Difaa El Jadid alithibitisha uwezo alionao kwa kufanya makubwa na milango ya kuonwa na timu nyingine ikafunguka.
“Huu ndio msimu bora kwangu na nimekuwa nikiukumbuka kila mara. Nautaja kuwa bora ulinifungulia milango ya kuaminiwa. Ulinifunza mengi ya nini napaswa kufanya ili kuendelea kulinda heshima ninayopata pia uliniongezea thamani kubwa,” alisema Msuva.
Katika msimu wa kwanza akiwa na timu hiyo alifunga mabao 11 na uliofuatia akafunga 13 ilhali ule wa tatu ambao hakuumaliza alifunga matano, kisha akajiunga na Wydad Casablanca pia ya Morocco na kuifungia mabao saba 2020/21 na matatu (2021/22) msimu ambao hakuumaliza.
“Sina maana kwamba baada ya kuhamia Wydad nilikuwa na msimu mbaya, ila timu hiyo ilikiona nilichofanya Difaa El Jadid, naamini hata nilipofika sasa ni kwa sababu ya CV niliyoanza kutengeneza timu hiyo,” alisema Msuva.
“Nimejifunza mambo mengi ndio maana sijawahi kukata tamaa. Nikipata changamoto nasimamia katika misingi ya kazi kuhakikisha nafanya mazoezi kwa bidii ambayo yataniweka fiti.”
Katika timu anayocheza Msuva amefunga mabao matatu katika mechi tatu.