TAAMULI HURU: Kilichofanyika mkutano mkuu wa CCM ni batili

Kilichofanywa na mkutano Mkuu wa CCM Dodoma, japo kimefanywa kwa nia njema na dhamira safi, lakini ni ubatili uleule kama uliofanywa na Bunge letu tukufu mwaka 2008 kwa kufanya mabadiliko batili ya Katiba kwa hati ya dharura na kuuchomekea ubatili kwenye Katiba yetu uliosababisha kutunga sheria batili ya uchaguzi.

Ule utaratibu wa CCM kupitisha viongozi kwa mtindo wa mserereko, ni utaratibu batili kinyume cha katiba ya CCM na kinyume cha Katiba ya nchi, kilichofanywa na mkutano mkuu wa CCM ni zaidi ya mserereko.

Kwa wale ambao hawakusoma safu yangu wiki iliyopita, msije kudhani mimi nawapinga viongozi wa CCM waliochaguliwa na mkutano mkuu, hapana, bali utaratibu uliotumika ndiyo huohuo uliotumiwa na Bunge kuchomekea ubatili kwenye Katiba yetu na kama hakutafanyika mabadiliko madogo ya Katiba, tunakwenda tena kwenye uchaguzi mkuu na sheria yenye ubatili.

Nilibahatika kuwepo Dodoma kwenye mkutano Mkuu wa CCM na kushuhudia kilichofanyika, hivyo kwanza; wiki iliyopita, niliungana na Watanzania wengine wote kuhakikishia Rais Samia Suluhu Hassan na timu yake, tuna imani kubwa sana na yeye na hatuna shaka na uwezo wake kuendelea, hivyo nilijiunga na wengine wote kumpongeza Rais Samia, kwa jinsi alivyoaminiwa na wana CCM hadi kuaminika na kumpitisha kwa kishindo kinyume cha Katiba ya CCM.

Lakini kwa sababu kilichofanyika kimefanyika kwa nia njema na dhamira safi, nilimpongeza Rais Samia, Dk Hussein Mwinyi, Dk Emmanuel Nchimbi na Mzee Stephen Wasira, kwa pongezi zangu za dhati, na leo hii ni mada ya kumpa ushauri, japo siyo lazima akubali kuufuata au kuutekeleza, lakini mimi nitakuwa nimetimiza wajibu wangu.

Kilichofanyika Dodoma katika mkutano mkuu wa CCM, kwanza ni halali kwa sababu mkutano huo una mamlaka yote ya kufanya jambo lolote au kuamua chochote, tatizo ni uamuzi huo kutofuata utaratibu, hivyo mwisho kuwa ni uamuzi batili.

Ibara ya 4 ya katiba ya CCM inasema Chama cha Mapinduzi kinaamini kwamba: Binadamu wote ni sawa. Hivyo wanaCCM wote ni sawa mbele ya chama. Ibara ya 7 inasema raia yeyote wa Tanzania mwenye umri usiopungua miaka 18, anaweza kuwa mwanachama wa Chama cha Mapinduzi.

Hii maana yake Chama cha Mapinduzi ni chama cha wote. Ile kauli kuwa CCM ina wenyewe, siyo kauli ya kweli, CCM ni chama cha wote.

Ibara ya 14 inazungumzia haki za wanachama, ikiwemo haki ya kuomba kuchaguliwa kuwa kiongozi wa CCM na ya kuchagua viongozi wake wa CCM kwa mujibu wa katiba, kanuni na taratibu za CCM.

Kwa ibara hiyo, inamaanisha ule utaratibu wa mserereko, ni utaratibu batili, unaofifisha haki za wanachama kugombea nafasi za juu za uongozi, na haupo mahali popote kikatiba ndani ya katiba ya CCM.

Kwa vile Rais Samia aliingia kwa kudra tu za Mwenyezi Mungu baada ya kifo cha mtangulizi wake, aliupata urais bila kusailiwa, na hii ni awamu yake ya kwanza, awamu yake ya pili ni ya 2025 – 2030 na kwa mujibu wa utaratibu wa CCM, kwa awamu ya pili ya urais, Rais aliye madarakani anapaswa kuendelea kupitishwa kugombea kwa utaratibu wa mserereko.

Kwa kuwa dhima ya mserereko ni kuepuka marudio (duplicity) kwa rais ambaye amekwisha sailiwa, lakini kwa vile Rais Samia hakusailiwa na kufuatia utendaji wake uliotukuka, wanaCCM katika umoja wao kupitia mkutano mkuu wao, wamempitisha kwa kauli moja kuwa ni yeye tu. Hata hivyo, upitishwaji huo haukufuata taratibu, ikiwemo kutengua kwanza kanuni, kwa mgombea kupitishwa bila kujaza fomu, bila kusailiwa na bila kupigiwa kura.

Japo kwa mujibu wa Ibara ya 100(2)ya katiba ya CCM, mkutano mkuu una mamlaka yote ya kufanya jambo lolote, mkutano mkuu wa CCM wa Taifa utakuwa ndicho kikao kikuu cha CCM kupita vyote na ndicho kitakachokuwa na madaraka ya mwisho.

Lakini kama hilo jambo limewekewa kanuni na utaratibu wa jinsi ya kufanyika, utaratibu wa kulifanya hilo jambo, uko kwenye Ibara ya 101 (4) inauruhusu Mkutano Mkuu, Kubadili sehemu yoyote ya Katiba ya CCM kwa uamuzi wa theluthi mbili za wajumbe walio na haki ya kupiga kura kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili kutoka Zanzibar. Pale Dodoma, sikubahatika kuona kura za bara na kura za Zanzibar, kutengua kwanza katiba, ndipo hilo lililofanyika likafanyika.

Pale Dodoma, hakukuwepo azimio lolote la kutengua kwanza kifungu chochote cha katiba ya CCM, taratibu na kanuni, kwa mujibu wa ibara ya 101 (4) ndipo azimio la kumpitisha kwa utaratibu mpya likapitishwa, pia sikuona kura za theluthi mbili za Bara na Zanzibar zikipigwa kutengua kanuni.

Kwa vile CCM kama chama tawala, ndicho kimeshika hatamu kuiongoza serikali, kama kinaweza kuikiuka katiba yake kwenye jambo kubwa kama hili, itakuwaje kwa katiba ya nchi? Bunge lilikiuka katiba na kuuchomekea ubatili ndani ya katiba, tusiiruhusu CCM kukiuka katiba yake.

Nini kifanyike? Katiba ya nchi ndiyo sheria mama ya nchi hii, katiba zote za vyama lazima zifuate sheria mama, ule utaratibu wa mserereko wa CCM, ni kinyume cha katiba ya nchi na kinyume cha katiba ya CCM, tunaomba Rais Samia aachane nao, asailiwe na utaratibu ufuatwe. Siku zote nimekuwa nikiwasisitiza wapinzani kujifunza kutoka CCM, lakini leo nashauri hakuna ubaya hata CCM ikijifunza mazuri kutoka kwa upinzani.

Nahitimisha kwa ule utangulizi, kumhakikishia Rais Samia kwamba Watanzania wanakupenda, wanakukubali, lakini usiruhusu ukiukwaji wa katiba ya CCM na katiba ya nchi kufifisha haki kuu ya kuchagua na kuchaguliwa, ruhusu haki kutendeka, utabarikiwa, CCM itabarikiwa na nchi itabarikiwa.

Related Posts