Trump Apingwa Suala La Kuwahamisha Wapalestina – Global Publishers

Makao makuu ya Al-Azhar jijini Cairo, Misri.

 

Taasisi ya Al-Azhar ya Misri, imelaani mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kuwatimua Wapalestina katika eneo la Ukanda wa Gaza, ikisisitiza kuwa, Ukanda wa Gaza ni ardhi ya Wapalestina na Waarabu na itabaki hivyo daima.

Taarifa iliyotolewa na Al Azhar imeutaja mpango wa Rais mpya wa Marekani, Donald Trump, wa kuwahamisha wakazi wa Ukanda wa Gaza na kuwapeleka katika nchi ya Misri na Jordan kuwa ni wa kidhalimu.

Al-Azhar imetoa wito kwa watu wa Palestina kupinga matakwa hayo ya kikatili na kidhalimu kwa kushikilia ardhi yao na kufungamana zaidi na malengo bora ya watu wa ulimwengu.

Al-Azhar imesema, kuwalazimisha Wapalestina kuhama nchi yao ni jaribio lililofeli na la kikatili la kutaka kuimarisha nafasi ya utawala wa Israel katika kupora ardhi na rasilimali zao, na kueleza kuwa baada ya kushindwa kunyakua ardhi kamili ya Palestina, sasa utawala wa Israeli umemua kutumia njia hiyo ya kidhalimu.

Umoja wa Ulaya pia umepinga mpango huo wa Trump wa kuwaondoa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na kuwahamishia Misri na Jordan.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas alisema juzi Jumatatu kando ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels kwamba watu wa Gaza wameteseka sana na wanastahili kuishi kwa amani kwenye ardhi yao.

Umoja wa Mataifa pia umepinga pendekezo la Rais mpya wa Marekani la kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amesema chombo hicho cha kimataifa kinapinga mpango wowote utakaopelekea Wapalestina kulazimika kuhama kutoka Ukanda wa Gaza au aina yoyote ya mangamizi ya kimbari.

Majuzi, Rais Donald Trump wa Marekani alitaka Wapalestina wa Ukanda wa Gaza wahamishwe katika ardhi yao na kupelekwa nchi jirani kama Misri na Jordan.

Related Posts