Uboreshaji daftari la wapigakura wafika Lindi

Lindi. Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge, na Madiwani Oktoba mwaka huu, Manispaa ya Lindi jana imeanza uboreshaji wa daftari la wapigakura na inatarajia kuandikisha wapigakura wapya 102,151 kutoka kwenye majimbo mawili ya uchaguzi.

Akizungumza leo Jumatano, Januari 29, 2025, Ofisa Muandikishaji wa Daftari la Wapigakura, Juma Mnwele, amesema Manispaa ya Lindi inatarajia kuandikisha wapigakura wapya 102,151, ambapo Jimbo la Mchinga wataandikisha 43,668 na Jimbo la Manispaa wataandikisha wapigakura 58,483.

“Lengo la kuboresha taarifa ni kwamba, kuna wengine wanaboresha taarifa zao kwa kuhama maeneo yao, kadi kupotea au majina yalikosewa, lakini kuna wengine watafutwa endapo wataonekana hawana sifa, kutokana na sababu mbalimbali kama vile, mtu aliyefariki na wengine kukana uraia wao,” amesema Mnwele.

Aidha, Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Zuwena Omary, amewaomba wananchi kujitokeza kujiandikisha ili ifikapo Oktoba watumie haki yao ya msingi ya kupiga kura kuchagua viongozi wanaofaa.

“Niwaombe wananchi wa Mkoa wa Lindi kujitahidi kwenda kujiandikisha ili wapate sifa ya kupiga kura hapo Oktoba 2025, ili kuwachagua viongozi wenye sifa,” amesema Omary.

Katibu Tawala mkoa wa Lindi, Zuwena Omary (mwenye gauni la bluu) na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva wakiwa kwenye foleni ya kwenda kujiandikisha. Picha na Bahati Mwatesa

Naye Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva, amewataka wananchi kuhamasishana kujitokeza kujiandikisha katika daftari la wapigakura, na watahakikisha wanafikia lengo la kuandikisha wapigakura wote wapya.

“Lengo la Manispaa ni kuhakikisha tunakwenda kuwaandikisha wapigakura wote wapya, niwaombe wananchi wa Manispaa ya Lindi kujitokeza kwa wingi ili tufikie malengo tuliyojiwekea,” amesema Mwanziva.

Sharifa Hassan, ambaye ni mlemavu wa macho, ameishukuru Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) kwa kuweka kipaumbele kwa watu wenye uhitaji.

“Naishukuru Tume ya Uchaguzi kwa kuweka kipaumbele kwa watu kama sisi tuliokuwa na ulemavu. Nimefika kituoni, sikupanga foleni, nikaingia ndani na kujiandikisha, nikapata kadi yangu ambayo itanisaidia kwenye uchaguzi mkuu kuchagua viongozi sahihi,” amesema Sharifa.

Jumla ya vituo 274 vitatumika kuandikisha wapigakura katika Manispaa ya Lindi, kazi iliyoanza Januari 28, 2025 hadi Februari 3, 2025.

Related Posts