Uongozi kituo cha afya Ilula waonywa wakipokea msaada wa gari la wagonjwa

Iringa. Uongozi wa Kituo cha Afya Ilula umeonywa kutobagua wagonjwa wanaohitaji kutumia gari la kubebea wagonjwa na kuhakikisha wananchi wote wenye uhitaji wanapata huduma bila kikwazo.

Hayo yamesemwa leo, Jumatano, Januari 29, 2025, na mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga, alipokuwa akikabidhi gari la kubebea wagonjwa kwa kituo hicho kilichopo Kitongoji cha Masukanzi, Kata ya Ilula, Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa.

“Ni muhimu kwa kila mwananchi kupata haki ya kulitumia gari hili bila kujali hali yake ya kiuchumi. Huduma za afya ni haki ya kila mtu, tunapaswa kuhakikisha zinawafikia wananchi wote,” amesema Nyamoga.

Amesema usafiri wa dharura na haraka ni muhimu katika kuokoa maisha ya mgonjwa, hivyo uongozi wa kituo hicho unapaswa kuhakikisha huduma hiyo inatolewa kwa usawa na kwa ufanisi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilolo, Anna Msola, amewaomba wananchi wa Kata ya Ilula kuonyesha ushirikiano na umoja katika kuwasaidia watumishi wa kituo hicho ili kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa zaidi.

“Tunapaswa kushirikiana na watumishi wa afya ili kuweka mazingira bora ya kufanya kazi, hivyo wananchi wote watanufaika na huduma za afya,” amesema Anna.

Mwenyekiti huyo amewataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za uongozi wa kituo cha afya, huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha ushirikiano na serikali ili lengo la kufikisha huduma za afya jirani na wananchi litimie.

Awali, Tabibu wa Meno katika Kituo cha Afya Ilula, Rachel Haule, alisema gari hilo ni la tatu kupokelewa Wilayani Kilolo, lakini ni la kwanza kupokelewa katika Kituo cha Afya Ilula, hivyo ni neema kwa kituo hicho.

Wakazi wa Ilula, akiwemo John Francis, wameelezea furaha yao baada ya kituo kupokea msaada wa gari hilo la kubebea wagonjwa, wakisema sasa wataepukana na changamoto za usafiri wa haraka pale mgonjwa anapohitajika kupelekwa kwenye hospitali kubwa.

“Haya maeneo ya wilaya yetu kuna wagonjwa wengi wanaotokea vijijini, huko hakuna hata magari. Gari hili litakuwa msaada mkubwa,” amesema John.

Hafla ya makabidhiano hayo imehudhuriwa na viongozi wa Serikali ya wilaya, wananchi, na watumishi wa afya wa Kituo cha Afya Ilula, ambapo gari hilo litakuwa chini ya usimamizi wa kituo hicho ili kutoa huduma kwa wananchi wa kata hiyo na maeneo jirani.

Related Posts