Unguja. Licha ya kaya 121 kuhitimu kutoka Mpango wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) katika Shehia ya Chumbuni Mkoa wa Mjini, zimeeleza jinsi utaratibu wa kuunda vikundi vya kuweka na kukopa unavyowanufaisha na kuimarisha maisha yao.
Kaya hizo zimepewa ruzuku za uzalishaji, Sh54,890 hadi kufikia Septemba mwaka 2024.
Kwa mujibu wa taarifa ya shehia hiyo iliyotolewa mbele ya wadau wa maendeleo waliotembelea kaya hizo katika shehia hiyo jana, Januari 28, 2028, walengwa wamepatiwa fursa za kuunda vikundi na jumla ya vikundi 12 vikijishughulisha na ujasiriamali tofauti.
Kupitia vikundi hivyo, jumla ya Sh19.35 milioni zimewekwa akiba, na kati ya hizo, Sh6.35 milioni zimetolewa mikopo kwa wanavikundi kwa kipindi cha mwaka 2022 hadi 2024.
Kaya hizo ambazo zilikuwa sehemu ya kaya 170 zilizokuwa kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini, zinajishughulisha na biashara ndogondogo, ufugaji na kilimo cha mbogamboga nyingi zikiwa kwenye vikundi.
Sheha wa shehia hiyo, Khamis Juma Juma, amesema mpango huo sio tu umebadilisha wananchi pekee, lakini umebadilisha sura nzima ya shehia kwani awali ilikuwa kama jangwa, lakini sasa baada ya kuanza utekelezaji wa miradi hiyo, imekuwa sehemu ya kipekee na kupanda miti ya matunda na mazao.
Amesema huduma za maji walikuwa wakizifuata eneo lingine, lakini sasa kuna visima tisa ambavyo vimechimbwa kupitia mpango huo.
“Hapa lilikuwa jangwa lakini kama mnavyoona tumepanda miti na mazao mbalimbali, wananchi wanaendelea kupata manufaa,” amesema.
Mmoja wa wahitimu katika mpango huo, Mchunga Ali Mbigili, amesema wakati anaingia kwenye mpango mwaka 2015 alikuwa akipata Sh36,000, lakini kadri zilivyokuwa zinaendelea, akaanza kujiwekeza na kufanya ujasiriamali.
Mwanamke huyo anayejishughulisha na ujasiriamali wa kushona nguo na mikoba, amesema alipata ruzuku ya Sh500,000 kisha akaanzisha biashara hiyo na kwa siku anapata wastani wa faida ya Sh20,000, ambayo anajiwekeza kwenye vikundi na kuweka akiba.
“Nimesomesha watoto wangu kwenye fedha hii, nasuka vikapu na kushona nguo, kwa kweli nimehitimu kutoka kwenye mpango, ila nashukuru tumepata faida kubwa na maisha yetu yameinuka,” amesema.
Wakati akisema hayo, mwingine, Keji Ali Juma, amesema aliingia kwenye mpango akiwa anapata Sh 61,000 lakini sasa amehitimu akiwa na mashine ya kuoka mikate na keki ambayo amekuwa maarufu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Shadrack Mziray, amesema kwa kawaida wamekuwa na mapitio ya utekelezaji kila baada ya miezi sita, hivyo wapo kwenye mapitio ya kawaida na wanaelekea katika kipindi cha mwisho kinachoishia Septemba mwaka huu.
“Kikubwa tulichoona leo ni mafanikio makubwa ambayo yamepatikana kuzinyanyua hizi kaya maskini. Wengi wao waliotoka kwenye mpango ni wale wanaopewa ruzuku ya kila baada ya miezi miwili, waliongezewa ya kuendeleza miradi yao ambayo ni wastani wa Sh 350,000.”
Amesema pamoja na programu hiyo licha ya kuelekea ukingoni, Serikali imekubali kuwapo na awamu nyingine ambayo ikianza utekelezaji wake itachukua wengine wanaohitaji baada ya wengine kuhitimu. Mpango unatarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu.
Naye mwakilishi kutoka Benki ya Dunia (WB), Claudia Zambra, amesema wanaridhishwa na namna mpango huo unavyotekelezwa na jinsi walivyoshuhudia miradi mbalimbali ya walengwa hao, huku Suzanne Keatinge kutoka ubalozi wa Ireland akipongeza jinsi mshikamano huo unavyoongeza tija kwa wananchi.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Salhina Mwita Ameir, amesema wananchi wanafarijika kwa miradi hiyo kama yalivyo malengo ya Tasaf yenyewe. “Kupunguza umasikini kuna njia nyingi, kuna kupunguza umasikini kupitia sekta ya elimu, afya, na fedha kwa kupata kipato pamoja na masuala ya kimazingira; yote lengo lake ni kuwawekea katika mazingira mazuri,” amesema.