Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema chama hicho kipo tayari kwa mazungumzo wakati wowote lakini hakiko tayari kuamrishwa.
Mbali na hilo, mwanasiasa huyo mkongwe, amemshauri Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kutumia 4R za Rais Samia Suluhu Hassan kuifanyia mabadiliko Chadema.
Wasira amesema hayo leo Jumatano, Januari 29, 2025 wakati akizindua maadhimisho ya miaka 48 ya CCM Mkoa wa Geita.
CCM ilizaliwa Februari 5,1977 baada ya kuungana Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP), cha Zanzibar.
“Walikuwa wanajisemea semea ooh ‘no reform no election’… alaa CCM ni chama kikubwa kuliko vyama vyote Afrika hatuwezi kuamrishwa…
“CCM tunamuambia sera yetu ya 4R iliyoasisiwa na Rais Samia tunakubali kuzungumza, wakihitaji waje tuzungumze, hatukatai kuzungumza lakini hatuwezi kuamrishwa; na hoja yenyewe wala haina msingi,”amesema Wasira.
Katika maelezo yake Wasira amesema anajua kuna watu wanamsema vibaya, “kuna mtu mmoja, huko ananisema ukikuta mtu anasema sema ujue sindano imemuingia mtu hawezi kusifu mvua kama haijawahi kumnyeshea.”
Wasira amesema miaka michache iliyopita Rais Samia alionesha njia ya kuzungumza na watu wote na vyama vyote na alifanya hivyo isipokuwa Chadema.
“Walikutana Dodoma wakakubaliana kuunda tume ya maridhiano kupitia mambo wanayoona yanaweza kurekebishika na walitoa mapendekezo waliyoyafikisha kwa Rais,” amesema.
Kuhusu Katiba, Wasira amesema CCM ilidai muda ulipo hautoshi lakini waingie kwenye uchaguzi kwa kurekebisha sheria na zote zimesharekebishwa.
“Chadema kama mdau aliitwa Dodoma kwenda kutoa mawazo yao, walienda watu wengi karibu watu 3,000 na madhahebu ya dini yote yaliwakilishwa,”amesema.
Wasira amesema Chadema na mabaraza yao ikiwamo Bawacha na Bazecha waligoma lakini maoni yaliyotolewa na vyama vingine na wadau waliliachia Bunge liamue na zikatungwa sheria kwa kuzingatia ushauri uliotolewa na vyama vya siasa.
“Chadema walikataa lakini kwa kuwa Rais wetu anapenda maridhiano akaunda kikosi cha watu watano kutoka CCM na watano kutoka Chadema juu ya mambo ambayo Chadema waliyaona yana manufaa,” amesema.
Wasira amesema katika mkutano huo, Chadema walipeleka mambo 11, kati ya hayo walikubaliana wajadili matano kwanza ikiwamo walilotaka watu waliokuwa uhamishoni warudi nchini.
Amesema Serikali ya Rais Samia iliridhia na kuwataka warudi nchini na wako salama jambo la pili walilodai kuna watu wao 400 wakati wa uchaguzi 2020 walibambikiwa kesi wakata zifutwe.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella alisema Serikali imefanya kazi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa sekta zote ikiwamo ya nishati na afya.
“Mkoa wetu ulikuwa na vijiji 350 vilivyokuwa na umeme kati ya vijiji 486 lakini sasa kati ya hivyo, 483 vimeshafikishiwa umeme na vilivyobakia viko kwenye visiwa na kuna mkandarasi anapeleka huduma hiyo kwa njia ya sola,” amesema.
Mbunge wa Geita, Joseph Kasheku ‘Musukuma’ amesema kulingana ubora wa utekelezaji wa Ilani ya chama hicho, walioufanya hawawezi kuuogopa uongozi wa Chadema hata kama kampeni zitaanza kesho.