Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga bw. Jastin Malisawa
Na Mwandishi wetu , Sumbawanga, Rukwa
Watanzania wameaswa kuuenzi urithi wa utamaduni usioshikika ili kuweza kurithisha mbinu za asili za kuhifadhi chakula na kuhifadhi mazingira ili kuwasaidia wakati wa majanga ya asili.
Wito huo umetolewa mjini Sumbawanga leo na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga bw. Jastin Malisawa wakati akifungua kikao kazi cha kutengeneza mwongozo utakaosaidia kuja na sheria ndogo ndogo za manispaa za kulinda urithi wa utamaduni usioshikika.
Kikao hicho kimeandaliwa na Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii (TAMCODE) na kujumuisha waheshimiwa madiwani, maafisa utamaduni mkoa wa Rukwa na wilaya ya Sumbawanga Machifu, na wanahabari.
Mustahiki Meya amesisitiza umuhimu wa kutumia mbinu za asili za kuhifadhi chakula na mapishi na kusema kuwa ni salama kwa afya kwani hazitumii kemikali jambo ambalo lilisaidia wazee wa zamani kuishi kwa miaka mingi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMCODE Bi. Rose Ngunangwa amesisitiza umuhimu wa kuja na sheria ndogo ambazo zitalinda maslahi ya wadau wa huduma na kazi za urithi wa utamaduni usioshikika ili kukuza vipato vya wanawake na vijana wilayani Sumbawanga.
Shirika la TAMCODE kwa kushirikiana na Mradi wa UNESCO- Alwaleed Philanthropies wameandaa vikao kazi mjini Sumbawanga, Mkoani Rukwa na wilayani Mpanda, Mkoani Katavi ili kuja na kanuni zitakazopelekea kutungwa kwa sheria ndogondogo za kulinda, kuhifadhi na kukuza urithi wa utamaduni usioshikika na kuchagiza ajira kwa vijana na wanawake kwenye wilaya hizo.
Mradi huo ulianza Novemba mwaka 2024 kwa kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa Redio Jamii na kidijitali katika mikoa hiyo.