Kigoma. Wastani wa watu 16 wakiwemo watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wajawazito hufariki kila wiki moja kutokana na ugonjwa wa malaria ndani ya kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
Akitoa takwimu hizo leo Jumatano, Januari 29, 2025, baada ya kupokea msaada wa vyandarua 5,000 pamoja na mahitaji mengine kwa ajili ya wakimbizi uliotolewa na Kampuni ya Itel Tanzania, Mkuu wa Kambi ya wakimbizi Nyarugusu, Siasa Manjenje, amesema malaria inachukua asilimia 40 ya magonjwa yote yaliyopo ndani ya kambi hiyo.
Amesema kwa miaka ya karibuni (2023/2024), ugonjwa wa malaria kambini ulishika kasi kutokana na uhaba wa fedha kutoka kwa wahisani, hali hiyo imesababisha huduma nyingi kambini kuzorota, ikiwemo huduma ya afya.
“Kama mnavyojua sisi kama Tanzania tumewahifadhi wakimbizi hawa lakini tunasaidiwa na mashirika ya kimataifa katika kuwapa huduma, na mashirika hayo yamepata uhaba wa fedha na kusababisha kupungua kwa huduma za afya, dawa, pamoja na vifaa tiba,” amesema Manjenje.
Amesema awali walikuwa na utaratibu wa kupuliza dawa katika maeneo mbalimbali ndani ya kambi hiyo ili kukabiliana na mbu wanaoambukiza ugonjwa wa malaria, ambapo kwa sasa dawa hiyo takribani miaka mitatu hajapulizwa, hivyo kusababisha ongezeko la maambukizi ya ugonjwa huo.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isack Mwakisu, akizungumza na Mwananchi kwa simu amesema jukumu la Serikali ni kuhakikisha ulinzi na usalama katika kambi hiyo.
Kuhusu uwepo wa malaria na idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo, amesema hana taarifa kamili, lakini atafuatilia ili kupata ufafanuzi zaidi.
Aidha, ameongeza kuwa nje ya kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, hakuna vifo vya watoto wachanga au wajawazito vinavyotokana na malaria kama inavyodaiwa kutokea ndani ya kambi hiyo.
Nao baadhi ya wakimbizi waliopokea mahitaji hayo wamesema wanaomba wadau wengine kujitokeza na kuwasaidia mahitaji muhimu, kwani ni mengi na Serikali na mashirika pekee hayawezi kumaliza tatizo kutokana na hali ya uchumi iliyopo kwao.
Naye Zabibu Bwenge, amesema vyandarua hivyo vitasaidia kupunguza vifo vya watoto wadogo na wajawazito vinavyosababishwa na malaria katika kambi yao, ingawa mahitaji bado ni makubwa.
“Vyandarua tulivyopokea leo ni vichache ukilinganisha na mahitaji ya watu, hivyo ni muhimu kuwapa vipaombele makundi maalumu kama watoto wadogo, wajawazito na wazee, na pia wadau waone umuhimu wa hili na kujitokeza kutusaidia,” amesema Mbogeka Matumaini.
Akizungumza wakati akikabidhi mahitaji hayo, Meneja Masoko wa Kampuni ya Itel Tanzania, Sophia Msafiri, amesema wameungana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), na kuiunga mkono Serikali kwa kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali ya takribani Sh100 Milioni.
“Sisi kama kampuni ya Itel hatujikiti tu katika masuala ya teknolojia, lakini tunajihusisha na masuala mbalimbali yanayohusisha jamii kwa kurudisha kwao kama shukrani, hivyo leo tumeleta vyandarua 5,000, kanga na vitenge 5,000, taulo za kike 5,000 pamoja na nguo za ndani za jinsia zote,” amesema Msafiri.
Kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu ina jumla ya wakimbizi 135,000 kutoka mataifa saba ya Afrika, ikiwemo nchi ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Uganda, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, na Sudan Kaskazini.