BAADA ya droo ya kupanga makundi ya fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 kukamilika, hapa kijiweni kwetu karibu wote tulikuwa tumeingiwa na ubaridi.
Kundi C ambalo tumepangwa kwenye Afcon 2025 ambazo zitafanyika Morocco sio mchezo na likatupa mchecheto sana kuanzia muda huo kwani tumepangwa na timu ambazo huwa zinatusumbua hasa.
Nigeria hatujawahi kuifunga hata mara moja katika mara zote nane tulizowahi kukutana hapo nyuma, imetufunga mara tano na tumetoka nayo sare tatu na wale Tunisia tumekutana nao mara mbili wakitufunga moja na tumetoka nao sare moja.
Uganda hao ndio wamejifanya wametuzoea sana maana inawezekana ndio timu iliyotufunga mara nyingi zaidi ambapo katika mechi 61 tulizowahi kukutana, jamaa tumewafunga mara 13 tu, tukipata matokeo ya sare mara 15 na mara 33 wametufunga.
Lakini baadaye tukaona hatuna sababu ya kukaa kinyonge kwa vile sisi timu yetu iliwekwa katika chungu cha mwisho kwenye tukio la upangaji wa makundi hayo hivyo hakuna namna ambayo tungeangukia katika kundi jepesi.
Katika mashindano kama Afcon usitegemee utakutana na mpinzani mwepesi na hautakiwi kucheza ili kukamilisha ratiba bali unapaswa ushindane haswa ili usigeuke mgawa pointi na badala yake ufike hatua za juu.
Hili ndilo tunataka kuliona kwa Taifa Stars pasipo kujali uwepo wa hizo timu ambazo hatuna historia nazo nzuri kwa maana kwamba tusigeuke vibonde wa kundi na kuwa daraja kwa wengine kusogea hatua zinazofuata.
Ili hilo lifanikiwe ni lazima kufanyike maandalizi ya kina kwa muda wa miezi 11 iliyobakia kabla ya kuanza kwa fainali hizo ambazo katika mara tatu zote tulizowahi kushiriki hapo nyuma tumeishia hatua ya makundi.
Maandalizi tutakayofanya ndio yatafanya tutambe ikiwa yatakuwa ya kiwango cha juu au yatatufanya tuchekwe ikiwa yatakuwa ya kubabaisha.