AKILI ZA KIJIWENI: Ikanga Speed afanye kazi hasa Yanga

JUMAMOSI iliyopita tulikuwa na hamu kweli ya kumuona bwana Jonathan Ikangalombo akiwa na jezi za Yanga katika mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Copco ambayo timu yake ilipata ushindi wa mabao 5-0.

Siku zote kipya kinyemi hivyo tukawa tunatamani kumuona kama vitu vimo mguuni au havimo maana kiutaratibu huku uswahilini, suala la kumjaji mchezaji kwa mechi moja ni la kawaida tu tukitembelea kauli ya ‘ukiujua umeujua’.

Kwa bahati mbaya, Ikangalaombo au Yanga wenyewe wanamuita Ikanga Speed, hakucheza mechi hiyo kwa kile ambacho kocha Sead Ramovic alikuja kukisema baadaye kuwa mchezaji wake mpya alikuwa mgonjwa.

Wahenga walisema subira ni ibada hivyo tunaendelea kusubiria tuone vitu vya Ikangalombo ambaye ameingia kuchukua nafasi ya Jean Baleke ambaye amefunguliwa mlango wa kutokea na Yanga.

Hata hivyo, pamoja na kwamba hajaanza kucheza, Ikangalombo ana shughuli pevu ya kufanya ili aweze kujihakikishia nafasi ya kucheza pale katika kikosi cha kwanza cha Yanga kutokana na uwepo wa mafundi kule mbele.

Ukisema atacheza upande wa wingi ya kulia kumbuka anatakiwa awanie namba na mzee wa kuchomekea Maxi Nzengeli ambaye anapokuwa uwanjani anaweza kukupa mabao, pasi za mwisho na akashuka chini kukaba, yaani ni mtu mwenye mapafu ya mbwa anayecheza uwanja mzima.

Akikimbilia wingi ya kushoto huko anaenda kukutana na kipenzi cha Wanajangwani, Stephane Aziz Ki ambaye amekuwa akiziamua mechi nyingi ngumu za timu hiyo hasa zile kubwa ambazo timu inahitaji matokeo mazuri.

Nafasi ya nyuma ya mshambuliaji wa kati ambayo pia Ikangalombo anaweza kuicheza, yupo bwana mkubwa Pacome Zouzoua ambaye anakupa burudani lakini pia anapiga pasi za mwisho na kufunga mabao.

Nikiwafikiria watatu hao huku nikikumbuka kuwa kwenye benchi kuna Clatous Chama anasubiria kuingia, naona kabisa kazini kwa Ikangaspeed kuna kazi.

Related Posts