TUMEWAONA Tabora United katika mechi 16 walizocheza kwenye Ligi Kuu msimu huu, walikuwa wa moto kweli na haikuwa rahisi kupambana nao ndani ya uwanja.
Walicheza soka la mipango na walionyesha kuwa wachezaji wao wanaelewa na kufanyia kazi vyema kile ambacho kocha wao Anicet Kiazayidi amekuwa akiwafundisha mazoezini.
Haikushangaza kuona warina-asali wakikusanya pointi 25 katika mechi 16 na hivyo kuweza kuwepo katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi nyuma ya vigogo Simba, Yanga, Azam na Singida Black Stars.
Unajua sio kazi rahisi kwa timu ya hadhi kama ya Tabora kukusanya pointi 25 katika mechi 16 za ligi kwani kwa ambao kidogo tumekuwa tukifuatilia Ligi Kuu Tanzania Bara kwa miaka kadhaa, kwa idadi hiyo ya mechi, timu nyingi huwa zinahangaika katika pointi 20 kushuka chini.
Sasa wakati gari la Tabora lilipoonekana limewaka na limeshashika kasi, ligi yetu ilisimama kwa muda kupisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi na baadaye ilikuwa ipishe fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) ambazo hata hivyo zilisogezwa mbele na hivyo kulazimisha ligi kurejea.
Wakati huo ligi inasimama pia ndio kilikuwa kipindi cha dirisha dogo la usajili na hapo Tabora ikaondokewa na baadhi ya wachezaji wake tegemeo wa kikosi cha kwanza kama kipa Musa Masalanga na kiungo Morice Chukwu ambao walichangia kuifanya timu hiyo kuwa imara mzunguko wa kwanza.
Kurejea kwa ligi kutatupa fursa ya kuona kama Tabora ilikuwa ni nguvu za soda, kubebwa na wachezaji wachache au kwamba ilikuwa na ubora wa kitimu uliowafanya wawe tishio mzunguko wa kwanza.
Timu nyingi za hadhi ya kati au chini kwenye ligi, zikipata mapumziko ya muda mrefu huathirika na huwa hazirudi katika ligi zikiwa na ubora wa awali pindi ligi ikirejea.
Mechi 14 zilizobakia kwa Tabora United kwenye ligi zinatosha kututegulia kitendawili hiki.