*Azindua Gereji ya St.Gabriel, chuo cha ushonaji na ufundi wa magari
*-Atoa mwito kwa wakazi wa Arusha kupeleka magari mabovu
Na Seif Mangwangi, Arusha
ASKOFU wa jimbo kuu Katoliki Arusha, Mhashamu Askofu Issack Amani amedai kuchukizwa na utoro wa vijana wanaopata nafasi ya kusomeshwa katika vyuo mbalimbali nchini ili kupata ujuzi na kuweza kuajiriwa na hivyo kutoa mwito kwa wazazi kuwa karibu na vijana wao kuwafunza maadili.
Aidha amewataka vijana wanaopata nafasi ya kusoma hususani ngazi ya ufundi katika vyuo tofauti nchini kuzingatia masomo yao kwa kuwa Wasomi ni wengi mtaani na ajira zimekua ngumu kupatikana.
Akizungumza jana Januari 29, 2025 wakati wa uzinduzi wa chuo cha ushonaji na chuo cha ufundi wa magari cha Mtakatifu Gabriel kinachoendeshwa chini ya kanisa Katoliki parokia ya Moyo Safi Unga Limited, Askofu Amani amesema wanafunzi wanapaswa kuwa wabunifu ili waweze kupata ajira.
Askofu Amani ambaye pia alizindua karakana ya kisasa ya kutengeneza magari inayojulikama kama ‘Mtakatifu Gabriel garage’ inayoendeshwa chini ya kanisa hilo hilo ametoa wito kwa wakazi wa ndani na nje ya Arusha kupeleka magari yao katika karakana hiyo kwa kuwa mafundi ni waaminifu na wanatoa huduma zenye ubora wa hali ya juu.
“Huko mtaani kuna vijana wengi sana wasomi wanazurura na vyeti vyao na hawana ajira kwa hiyo nipende kutoa wito kwa vijana wanaopata nafasi ya kusoma kuwa makini na masomo lakini pia wawe wabunifu ili kuwafanya waweze kuajirika,”amesema.
Amesema lengo la kufunguliwa kwa vyuo hivyo ni kufungua matumaini kwa vijana wanaotoka kwenye familia masikini na kuonya vijana ambao wamekuwa wakifanya uzembe kuchukuliwa hatua kwa kuwa kinachofanyika hapo ni kuwajengea ujuzi watakaotumia kuendesha maisha yao.
Aidha amezitaka bodi zinazosimamia vyuo hivyo kuwa wakali kwa watendaji ili kuvifanya vyuo hivyo kuwa bora ndani na nje ya Arusha na kuvifanya kuwa endelevu lakini pia kuwa wabunifu kuhakikisha vyuo hivyo vinaleta ushindani dhidi ya vyuo vingine.
Askofu Amani amesema karakani ya Mtakatifu Gabriel ilianzishwa mwaka 2004 lakini ilikufa kutokana na kutokuwepo kwa usimamizi madhubuti na kanisa la Moyo safi lilipofika ofisini kwake kuomba lipewe karakana hiyo kuiendesha aliwakubalia na wameonyesha wanaweza.
“Karakana hii ilikuwepo lakini kilichoiangusha hapo mwanzo ni usimamizi mbovu, lazima bodi iwe makini kusimamia na kuifanya kuwa endelevu, kila kinachofanyika ni lazima kitolewe ripoti na ukaguzi ufanyike kila mara, isijekutokea vipuri vya magari vinaisha dukani mahesabu hayaonekani ukiuliza unakosa majibu hiyo sio sahihi kabisa,”amesema Askofu Amani.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia ya Moyo Safi na msimamizi mkuu wa miradi hiyo, Padre Festus Mangwangi amesema kwa muda wa wiki mbili kuanzia Januari 29,2025 wakazi watakaopeleka magari yao kutengenezwa hawatatozwa gharama yoyote ya matengenezo.
“Kwa kuwa gereji yetu ni mpya tunatoa ofa kwa yoyote atakayeleta gari lake kwaajili ya matengenezo au kufanyiwa service hatotozwa kiasi chochote cha fedha, ofa hii ni ya muda wa wiki mbili na baada ya hapo wiki mbili zingine tutawatoza nusu bei,”amesema.
Awali akisoma risala ya Moyo safi wa bikira maria, Katibu wa Parokia hiyo, Arsen Akaro amesema ukarabati wa chuo hicho umegharimu zaidi ya Milioni 150 ambazo zimetokana na michango ya wanaparokia ya Moyo safi.
Amesema chuo hicho ambacho kimeanzishwa rasmi Aprili 1, 2024 baada ya ukarabati kukamilika, kimepata mafanikio makubwa ikiwemo kupokea wanachuo 53, 10 wakiwa ni wasichana na 43 wavulana, na kwamba wengi wao ni darasa la saba na baadhi kidato cha nne na wote wanasomea mtaala wa VETA.
“Baba Askofu fani zinazofundishwa chuoni hapa ni pamoja na ufundi magari, ufundi wa kuchomea, kunyoosha na kupaka rangi na umeme wa magari, tumeshatangaza kupokea tena wanafunzi na tayari tumepokea wanafunzi 7 na wameanza masomo,”amesema Akaro.
Kuhusu chuo cha ushonaji, Akaro amesema chuo hicho kilichoanzishwa Mei 15, 2024 kina wanafunzi 48 wote wakiwa wanawake kinakabiliwa na changamoto kubwa ya wanachuo kushindwa kuchangia gharama kidogo ya TZS 1000 kwa siku kutokana na kwamba wengi wao wametoka kwenye familia masikini .
Amesema mishahara ya wakufunzi pamoja na chakula cha wanafunzi hao kilikuwa kikigharamiwa na shirika la WINGAD lililopo chini ya Jimbo katoliki Arusha na kwamba ufadhili wake uliisha Disemba mwaka jana.
Padre Festus Mangwangi Paroko wa parokia ya Moyo safi Unga Ltd akitoa maelezk mafupi kuhusu chuo cha ufundi na gereji ya Sr.Gabriel na chuo cha ushonaji kwa Askofu Isack Amani wakati wa halfa ya uzinduzi wa vyuo hivyo jana