Azimio la Dar na mustakabali wa uchumi Tanzania, Afrika

Azimio la kuchochea upatikanaji wa nishati ya uhakika na nafuu Afrika, linatajwa kuwa chachu ya kuvutia uwekezaji, ongezeko la viwanda na hatimaye kukua haraka kwa uchumi wa mataifa ndani ya bara hilo.

Kwa mujibu wa wadau wa nishati na uchumi, kuna uhusiano wa karibu kati ya ukuaji haraka wa uchumi unaochochewa na uwekezaji wa viwanda na kuwepo kwa nishati nafuu na ya uhakika.

Hilo linathibitishwa pia na ripoti ya Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) ya mwaka 2023, inayoonyesha upatikanaji wa nishati ya uhakika umeongeza uzalishaji katika viwanda vya kilimo na ujenzi kwa zaidi ya asilimia tano katika nchi za Afrika Magharibi, ikiwemo Ghana na Ivory Coast.

Kwa sababu ya uhalisia huo, wakuu wa nchi 21 za Afrika walikutana Dar es Salaam, Januari 27 na 28 mwaka huu, kujadili kuhusu nishati ya umeme na kuazimia mambo mbalimbali, hatua iliyowaibua wadau waliosema ni fursa ya kukua kwa uchumi.

Katika azimio la pamoja la wakuu hao wa nchi, walikubaliana kuwa nishati ni nyenzo muhimu ya kutokomeza umasikini, kuchochea ujenzi wa viwanda, hivyo ni muhimu kuboresha miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wake.

Suala la kutengeneza usawa wa kutafuta fedha za kuimarisha mifumo na mipango ili kurahisisha gharama za nishati ni jambo lingine lililoridhiwa na wakuu hao wa nchi katika Azimio la Dar es Salaam.
Kadhalika, wamekubaliana kutenga bajeti za ndani na kuziunganisha na msaada wa fedha kutoka kwa wadau wa kimataifa katika kutekeleza mipango ya uimarishaji upatikanaji wa nishati.

Mkutano huo, ambao chimbuko lake ni Benki ya Dunia na AfDB, ulilenga kusaka mustakabali wa nishati Afrika na kujiwekea lengo la kuwafikishia huduma hiyo wakazi milioni 300 wa bara hilo ifikapo 2030, kati ya milioni 600 waliopo gizani sasa.

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utu na Mazingira (Hudefo), Sarah Pima anasema kinachohalalisha nchi kuitwa imeendelea ni kuwa na nishati bora, ya uhakika na rahisi kwa watu wake.
Anasema kwa kuwa Azimio la Dar es Salaam pamoja na mambo mengine linalenga kufanikisha usambazaji wa nishati Afrika, hivyo uchumi wa mataifa ndani ya bara hilo utafunguliwa.

Kufunguliwa kwa uchumi huo kutatokana na kile alichosema, kuwepo kwa nishati kunachochea ongezeko la shughuli za maendeleo, lakini kuwezesha uwekezaji hasa wa viwanda.
Iwapo shughuli za uchumi zitaongezeka na wawekezaji watawekeza hasa katika ujenzi wa viwanda, anasema Tanzania na hatimaye Afrika itaimarisha uchumi wake na hata wa mwananchi mmojammoja.

“Kunahitajika kuhakikisha kunakuwa na mipango thabiti, ushirikiano na ujumuishi wa wadau, ikiwemo sekta binafsi, wanawake, vijana na asasi za kiraia, mambo yote hayo yametajwa ndani ya azimio hilo,” anasema.

Sarah anasisitiza umuhimu wa kuwa na njia nzuri za kifedha kutekeleza azimio hilo, ili kusiwe na nafasi tena ya kuzungumza, badala yake mataifa yajikite na utekelezaji.

“Imeshatosha kujadili ni muda wa utekelezaji na kuchukua hatua. Jitihada zikibebwa na Afrika kwa ujumla wake, itasaidia kufikia malengo kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza,” anaeleza.

Mkuu wa Matawi ya Kimataifa wa Benki ya Standard Chartered, Lewis Mlay anasema azimio hilo litachochea uzalishwaji wa ajira na hatimaye kukua kwa pato la taifa.

“Kwa sababu kuwepo kwa nishati ya kutosha kutaongeza shughuli za kiuchumi na hata umasikini utapungua au kwisha kabisa kwa Watanzania na Waafrika kwa jumla,” anasema.
Mlay anahusianisha utekelezwaji wa azimio hilo na kufanikishwa kwa lengo la Tanzania la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Binafsi naona lile lengo la kufikisha asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi litawezekana iwapo kutakuwa na nishati ya uhakika kama wakuu wa nchi walivyoazimia,” anaeleza.
Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Mark Mwandosya anaeleza nyenzo ya ukuaji haraka wa uchumi wa taifa lolote Afrika na duniani ni uwekezaji kwenye viwanda.

Anasema ni vigumu kumshawishi mwekezaji wa kiwanda kuwekeza katika taifa lisilo na nishati ya uhakika, itamuingiza kwenye gharama kubwa za uzalishaji.

Na kwa sababu Azimio la Dar es Salaam linalenga kuwezesha upatikanaji wa nishati Afrika, anasema wawekezaji kutoka nje ya bara hilo watavutiwa kuwekeza Afrika na hatimaye kukuza uchumi.
Kwa mujibu wa Profesa Mwandosya, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), viwanda vinazalisha ajira na kuingiza mapato kwa taifa.

“Panapokuwa na kiwanda, nchi inaingiza kwa kukusanya mapato, wananchi wanaingiza kwa kufanya kazi, lakini wakati mwingine kuuza malighafi, kama kiwanda cha kilimo, mazao yatapata soko. Katika mazingira haya, uchumi unakua kwa kasi,” anasema.

Anasema iwapo yaliyoazimiwa yatasimamiwa na kutekelezwa kama inavyopaswa, Afrika litakuwa bara la mfano na litatimiza lengo lake la muda mrefu la kujitegemea.

Mhandisi na Mshauri wa Nishati Jadidifu, Matthew Matimbwi anasema azimio hilo kwanza, linafungua milango ya uendelezaji wa nishati jadidifu, pili linaipa nafasi nchi ya kuridhia teknolojia mbadala zinazohusu nishati.

Kwa sababu ni muda mrefu Serikali imejikita katika uzalishaji umeme wa kutumia vyanzo vinavyoathiriwa haraka, anasema azimio hilo linaondoa utaratibu huo.

“Serikali imejikita kwenye uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji, hii ni teknolojia iliyowaingiza kwenye giza majirani zetu Zambia. Mto Zambezi umekauka kwa sababu ya ukame wamejikuta gizani. Sisi tuna uhakika gani kama Bwawa letu la Julius Nyerere litakuwa na maji miaka yote,” anasema.

Matimbwi, ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (Tarea) anasema kilichotokea Zambia kinatuma ujumbe kwa Tanzania kuhusu usalama wa nishati yake.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, azimio hilo linaipa nafasi nchi kuridhia mikataba ya uzalishaji wa nishati kwa kutumia teknolojia jadidifu kwa maana tungamotaka, jua, upepo na joto ardhi utapata nafasi.

“Tarea imekuwa ikishauri vitu vingi vifanyike, lakini kulikuwa na ukakasi wa utekelezaji, lakini azimio hili linakwenda kuchochea utekelezaji,” anaeleza. Pamoja na hayo, anasema kilichoazimiwa kinatoa fursa ya kufanya uzalishaji wa nishati kwa usalama wa mazingira.

“Kuna wananchi kwa uchumi wao itachukua muda mrefu kununua nishati za kupikia ambazo kila siku zinahitaji fedha. Unakumbuka mitungi ya gesi iligawiwa bure, lakini wengi ilipoisha gesi waliishia kuacha kuitumia,” anasema.

Kinachohitajika, anasema ni mwananchi aachwe aendelee kutumia kuni, isipokuwa kuwepo teknolojia itakayopunguza kiwango cha athari kwa chanzo cha nishati anachotumia.
Anasema matumizi ya nishati jadidifu ni rahisi, salama na uhakika, hivyo nchi itaendelea kiuchumi kwa kuwa hata wananchi hawatatumia gharama kubwa kupata nishati.
 

Akizungumza katika mdahalo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Fedha la Benki ya Dunia (IFC), Makhtar Diop alisema umefika wakati sasa kwa nchi za Afrika kuacha kuona umeme kama sekta ya kimkakati inayopaswa kuzalishwa na Serikali, badala yake ialike sekta binafsi.

“Tunapaswa kuhusisha sekta binafsi katika utafutaji fedha kwa ajili ya usambazaji umeme na uzalishaji, tubadili mifumo iliyozoeleka na kuruhusu vyanzo mbalimbali vya fedha kama mifuko ya pensheni na mifuko ya hifadhi ya jamii kugharimia miradi ya usambazaji wa umeme,” alisema.

Katika hili alisema mbali na kuita sekta binafsi kwa ajili ya kuwekeza katika uzalishaji wa umeme, ni muda wa kuangalia namna gani umeme huo utafika kwa wananchi kwa kuwa kampuni nyingi hazina uwezo wa kusimamia usambazaji umeme.

“Kwa Afrika wengi wanawekeza katika uzalishaji, lakini hakuna ufungamanishaji mzuri kati ya kuzalisha na kusambaza, hivyo tunahitaji kuwa na kampuni zitakazojiwekeza katika kusambaza umeme peke yake,” alisema.

Naye Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa TotalEnergies, Patrick Pouyanné alisema ni wakati sasa kwa nchi za Afrika kuanza kuwekeza katika mifumo ya kusambaza nishati kwa kuwa zinapokuwa na mikakati ya kuzalisha nishati jadidifu ni lazima umeme huo kuunganishwa katika gridi.
“Leo hii ukisema uwe na kampuni inayosafirisha na kufanya ugavi si rahisi kwa sababu ni mtaji mkubwa unahitajika ili kukamilisha hilo,” alisema.

Alisema kukosekana kwa mifumo imara ya usambazaji umeme, inaweka ugumu katika kuvutia uwekezaji wa kimataifa na binafsi katika uzalishaji.

Related Posts