Banda, Mukrim wampa jeuri Mecky Maxime

KOCHA wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime ametaka Ligi Kuu Bara ianze hata sasa baada ya kupata jeuri kutokana na kuongezewa nguvu kwa usajili wa mabeki wawili wa kati, Mukrim Issa kutoka Coastal Union na Abdi Banda aliyekuwa anacheza Richards Bay ya Afrika Kusini.

Maxime alisema usajili huo umezingatia mahitaji ya kuongeza nguvu eneo la ulinzi, kuhakikisha mzunguko wa pili unakuwa wa kutimiza malengo yakiwamo ya kumaliza ndani ya nafasi tano za juu katika msimamo wa  Ligi Kuu.

“Tumesajili wachezaji wawili kupitia dirisha dogo kwa sababu nilihitaji kila nafasi iwe na ushindani, jambo jingine nimezingatia uzoefu na uwezo wao, utaongeza nguvu katika mapambano yetu,” alisema Maxime na kuongeza;

“Mzunguko wa pili unakuwa na ushindani na wa malengo mazito kwa kila timu. Kwa upande wetu tupo tayari kukabiliana na ushindani kwa mechi zilizobakia mbele yetu.”

Alisema baada ya mapumziko ya ligi wanarejea kazini ili kumalizia msimu na anaamini wachezaji wake watafanya kazi nzuri ya kukamilisha malengo waliyojiwekea.

Katika mechi 16 ilizocheza Dodoma, imeshinda tano, sare nne na imefungwa saba ina pointi 19, jambo ambalo Maxime alisema wanahitaji kupanda nafasi za juu.

“Haiwezi kuwa kazi rahisi ila inawezekana, ndio maana nasema wachezaji wapo tayari kwa mapambano, hao mabeki wawili pia wanajua nini wanapaswa kukifanya katika timu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Kagera Sugar aliyewahi kuzitumikia Mtibwa na Taifa Stars kwa miaka 10 mfululizo.

Kwa upande wa Banda, anayemudu kucheza beki wa kushoto, kati na hata kiungo mkabaji alisema kurejea kwake kwa mara nyingine Ligi Kuu, anatambua atahitaji kujituma ili kiwango chake kiwe msaada kwa timu hiyo.

“Nafahamu mashabiki watakuwa wananitazama kwa jicho la nitafanya kitu gani, baada ya kurejea kutoka Afrika Kusini, mimi ni mtu ambaye siogopi kuanza nilipoishia, hiyo siyo mara ya kwanza kufanya hivyo,” alisema.

Related Posts