FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Raphael Chibunda, amewataka wanafunzi waliopata ufadhili wa masomo kutoka taasisi ya CAN TANZANIA kuzingatia masomo na kuwa na nidhamu ili waweze kufikia malengo yao ya kielimu.
Prof. Chibunda ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaofadhiliwa na taasisi ya CAN TANZANIA. Alisisitiza kuwa SUA ni moja ya vyuo vilivyopokea ufadhili huo na akaihimiza taasisi hiyo kupanua wigo wa utoaji wa ufadhili ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wanaohitaji msaada wa kifedha ili kuendelea na masomo yao.
Mwenyekiti wa Bodi ya CAN Tanzania, Dkt. Catherine Aloyce Masau, amesema kuwa shirika hilo limefadhili wanafunzi 36 kutoka vyuo mbalimbali nchini, ikijumuisha Tanzania Bara na Zanzibar. Ufadhili huo umetolewa kwa ngazi mbalimbali za elimu, ikiwemo shahada ya uzamili, diploma, pamoja na cheti. Amesisitiza kuwa ufadhili huo umewalenga wanafunzi wa jinsia zote, wakike na wakiume, hasa wale wanaotoka kwenye familia zisizojiweza.
“Watanzania wengi hawana uwezo wa kumudu gharama za masomo na wanategemea ufadhili kutoka serikalini. Kama CAN Tanzania, tumeona umuhimu wa kusaidia serikali kwa kupitia mpango huu wa ufadhili,” alisema Dkt. Catherine. Alitoa wito kwa wanafunzi walionufaika na ufadhili huo kusoma kwa bidii ili elimu wanayoipata iweze kuwanufaisha wao na jamii wanayotoka
Mkurugenzi Mkuu wa CAN Tanzania, Dkt. Sixbert Mwanga, alieleza kuwa moja ya vigezo muhimu vya mwanafunzi kupata ufadhili ni lazima awe ametoka kwenye familia yenye hali duni na pia kozi anayosomea iwe inahusiana moja kwa moja na huduma kwa jamii. Aidha, alisisitiza kuwa mwanafunzi anayepata ufadhili ni lazima aonyeshe ufaulu mzuri ili kuendelea kunufaika na mpango huo.
Ampelius Anthony, mwanafunzi wa Tiba ya Mifugo kutoka SUA, ni mmoja wa walionufaika na ufadhili huo. Alieleza kuwa safari yake ya elimu ilikuwa na changamoto kubwa kiasi cha kulazimika kuomba msaada wa walimu wake ili aweze kuendelea na masomo.
“Ufadhili huu umekuja wakati sahihi kwangu na utanisaidia kutimiza malengo yangu ya kielimu,” alisema mwanafunzi huyo.
Aidha, alieleza kuwa wapo wanafunzi wengine aliokuwa anasoma nao ambao walishindwa kuendelea na masomo kutokana na changamoto za kifedha. Alitoa wito kwa taasisi nyingine kuiga mfano wa CAN Tanzania kwa kusaidia wanafunzi wenye uhitaji ili waweze kufanikisha ndoto zao za kielimu.
Kwa ujumla, mpango huu wa ufadhili wa masomo kutoka CAN Tanzania unazidi kuwa nuru kwa wanafunzi wengi nchini, huku ukichochea ari ya bidii katika masomo na kuwawezesha vijana wa Kitanzania kujenga mustakabali mzuri wa maisha yao.