DC Mufindi atahadharisha kuhusu ugonjwa wa Marburg

Mufindi. Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa wamewataka wananchi katika wilaya yake kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Marburg ambao umeripotiwa kuingia hapa nchini katika Wilaya ya Bihalamuro mkoani Kagera.

Januari 20, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alithibitisha uwepo wa ugonjwa huo wakati alipoungumza na waandishi wa habari akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya duniani (WHO), Dk Tedros Adhanom, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma. 

Licha ya kuwepo kwa ugonjwa huo, Serikali imefanikiwa kuudhibiti mapema na hadi sasa wote waliohisiwa walipimwa na hawakukutwa na maambukizi ya virusi vya Marburg huku kesi mbili zikiripotiwa.

Dk Salekwa ametoa wito huo leo Januari 30, 2025 wakati akizungumza na wadau kuhusu mapendekezo ya Rasimu ya Mapango wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Mufindi (DCC) kilichofanyika katika ukumbi wa boma mjini Mafinga.

Amesema, kama wilaya, wamechukua hatua mbalimbali mapema kwa ajili ya kudhibiti ikiwemo kutoa elimu ya kupambana na suala hilo.

Ameongeza kuwa lengo la kutoa taadhari hiyo ni kila mtu awe na uelewa hasa namna unavyoambukiza pamoja na dalili zake huku akiwataka waendelee kumwomba Mungu kuhusu ugonjwa huo.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Mfinga, Dk Bonaventura Chitopela amesema kila mmoja ana wajibu wa kuchukua taadhari hiyo, siyo kwa wataalamu wa afya pekee, bali hata wananchi kujua kinachosababisha kuenea kwa ugonjwa huo na namna ya kujinga.

“Kwa sasa tumetoa mafunzo kwa wataalumu wa afya kujua maana ya ugonjwa huu na unasababishwa na kitu gani, unavyoenea pamoja namna ya kujikinga,” amesema Dk Chitopela.

Ameongeza kuwa: “Sisi kama waganga wakuu tunahakikisha tunajiandaa kwa lolote linaloweza kutokea kwa sababu tayari wenzetu wa Mkoa wa Kagara wameshapata, ukizingatia Mafinga tupo barabarani na tunapokea wageni wengi, hivyo lazima tujiandae.”

Dk Chitopela amesema kuwa tayari wameandaa maeneo endapo mgonjwa akitokea mwenye dalili kama hizo watamtenga na kumhudumia.

Pia, Mganga Mkuu huyo wa Mafinga ameyataja maeneo yao ambayo wameyatenga kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa hao kuwa ni Kituo cha Afya cha Upendo, Kituo cha Afya Ifingo pamoja na Zahanati ya Changalawe.

Hata hivyo, Dk Chitopela ameeleza sababu za kutenga maeneo hayo kuwa eneo la Upendo lipo mwisho huku maeneo mengi yatakuwa ya kwanza endapo ikitokea kwa sababu yapo pembezo mwa Mji ikiwa Changalawe na Ifingo.

Related Posts