Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imeielekeza Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam kushughulikia dhamana ya mwanasiasa maarufu nchini, Dk Wilbrod Slaa, na kutoa uamuzi wa pingamizi la uhalali wa kesi ya jinai inayomkabili kwa haraka.
Mbali na maelekezo hayo kwa Mahakama ya Kisutu, pia kupitia sakata la dhamana ya mwanasiasa huyo, Mahakama Kuu imetoa maelekezo maalumu kwa mahakama zote za chini kuhusu namna ya kushughulikia dhamana za washtakiwa wa kesi za jinai.
Katika maelekezo hayo, Mahakama Kuu imezitaka mahakama hizo kuweka kipaumbele cha kwanza kushughulikia dhamana kuliko masuala mengine yanayohusiana na kesi hizo. Pia, imesisitiza kuwa suala la dhamana linapaswa kushughulikiwa siku ya kwanza mshtakiwa anaposomewa mashtaka.
Mahakama Kuu, kupitia uamuzi wa mashauri mawili ya maombi ya Dk Slaa, leo Alhamisi, Januari 30, 2025 imetoa maelekezo maalumu kwa Mahakama ya Kisutu na mahakama nyingine za chini kushughulikia dhamana kwa haraka.
Dk Slaa, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu 2010, alifungua mashauri hayo kutokana na mwenendo wa kesi ya jinai inayomkabili katika Mahakama ya Kisutu.
Katika mashauri hayo, mbunge huyo mstaafu wa Karatu aliomba mahakama iitishe na kupitia mwenendo wa shauri dogo lililofunguliwa na Jamhuri kupinga dhamana yake—pamoja na kesi ya msingi—ili kujiridhisha na usahihi na uhalali wake.
Mashauri hayo yote yalisikilizwa na Jaji Kirekiano—moja Alhamisi na jingine Ijumaa ya wiki iliyopita.
Katika shauri la dhamana, mawakili wa Dk Slaa, pamoja na mambo mengine, walidai kitendo cha Mahakama ya Kisutu kuahirisha mwenendo wa shauri la Jamhuri kupinga dhamana na kuamuru Dk Slaa apelekwe mahabusu kusubiri kusikilizwa kwa shauri hilo hakikuwa sahihi.
Kutokana na hilo, mawakili wake—Peter Madeleka, Hekima Mwasipu, Edson Kilatu, na Paul Kisabo—waliiomba mahakama ifute mwenendo wa shauri hilo na kumpa dhamana mteja wao.
Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa vikali na jopo la mawakili wa Serikali likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, ambaye pamoja na mambo mengine, alidai kuwa hakukuwa na ukiukwaji wa sheria na taratibu katika uahirishwaji wa shauri hilo, na kwamba ulifanyika kwa mujibu wa sheria.
Kuhusu shauri la uhalali wa kesi inayomkabili Kisutu, mawakili wa Dk Slaa walidai kuwa kesi hiyo ni batili na inapaswa kufutwa kwa kuwa ilifunguliwa kinyume cha Kifungu cha 131A(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kama ilivyorekebishwa mwaka 2022.
Kifungu hicho kinakataza kufungua mashauri mahakamani kabla ya kukamilika kwa upelelezi, isipokuwa kwa makosa makubwa yanayoorodheshwa katika kifungu kidogo cha 4 cha sheria hiyo.
Hata hivyo, Wakili Katuga alipinga hoja hizo akidai kuwa Mahakama hiyo si mahali sahihi kuwasilisha malalamiko dhidi ya hati ya mashtaka kwa kesi iliyoko Mahakama ya Kisutu.
Alifafanua kuwa awali walishawasilisha malalamiko hayo Mahakama ya Kisutu na wakasikilizwa, lakini kabla ya uamuzi kutolewa, wakafungua shauri la madai hayo hayo Mahakama Kuu.
Aliongeza kuwa kuhoji uhalali wa mashtaka kunagusa mamlaka ya mahakama kusikiliza kesi husika, na kwamba mahakama ya chini yenyewe ina mamlaka ya kusikiliza na kuamua malalamiko hayo.
Katika uamuzi wa shauri la dhamana, Jaji Kirekiano amesema ni wajibu wa mahakama kisheria na kikatiba kutoa haki kwa haraka.
Baada ya kupitia mwenendo wa shauri dogo la Jamhuri kupinga dhamana ya Dk Slaa, hakuona sababu za msingi za Mahakama ya Kisutu kuahirisha bila kushughulikia suala la dhamana.
Kwa hiyo, Jaji Kirekiano ametoa maelekezo mbalimbali kwa ajili ya kuboresha mwenendo wa mashauri yenye mazingira kama hayo.
Kwanza, amesema kuwa dhamana ni haki ya msingi, na kwa mujibu wa dhana ya kutokuwa na hatia hadi itakapothibitishwa mahakamani, dhamana inapaswa kushughulikiwa siku ya kwanza mshtakiwa anapofikishwa mahakamani, isipokuwa kwa sababu maalumu zinazopaswa kurekodiwa katika mwenendo wa shauri.
Jaji Kirekiano ameongeza kuwa, pale ambapo kuna pingamizi dhidi ya dhamana, mahakama inapaswa kushughulikia suala hilo kwa haraka zaidi, kwa kuwa linahusu uhuru wa mtu binafsi.
Kuhusu shauri la uhalali wa mashtaka, Jaji Kirekiano amesema Mahakama ya Kisutu ilishapanga kutoa uamuzi wake Januari 23, na kwa kuwa ina mamlaka ya kushughulikia shauri hilo, inapaswa kufanya hivyo bila kuchelewa.
Baada ya uamuzi huo, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye pia ni mwanasheria, ameungana na jopo la mawakili wa Dk Slaa mahakamani kupokea uamuzi huo.
Nje ya Mahakama, Lissu amesema kuwa Mahakama Kuu imetoa maelekezo mazuri kuhusu umuhimu wa dhamana kama haki ya msingi ya mshtakiwa.
Kwa upande wake, Wakili Madeleka amesema wanatarajia Mahakama ya Kisutu na mahakama nyingine zote za chini kuheshimu maelekezo hayo na kutambua kuwa dhamana ni haki ya mshtakiwa.
Hata hivyo, kuhusu uhalali wa mashtaka amesema kuwa Mahakama Kuu kuiachia Mahakama ya Kisutu kutoa uamuzi wake iliokuwa imeuandaa, wanaona kuwa Mahakama Kuu imekwepa wajibu wake kwani inayo mamlaka ya kuingilia suala lolote bila kujali chochote kinachoendelea huko chini.
Wakili Mwasipu amesema sasa wanakwenda Mahakama ya Kisutu kuomba amri ya kumfikisha mahakamani mteja wao ili kutoa uamuzi kama Mahakama Kuu ilivyoelekeza.
Wakati akitoka mahakamani akielekea kupanda gari la Magereza kurejeshwa mahabusu, Dk Slaa aliwapungia mkono watu waliojitokeza mahakamani kuwashukuru, huku huo akiwataka wasioge kwa madai kuwa hizo ni hatua za ukombozi.
Katika kesi ya msingi namba 993/2025—Dk Slaa anakabiliwa na shtaka la kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa X (zamani Twitter), kinyume cha Kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao Namba 14 ya mwaka 2015.
Anadaiwa kuwa Januari 9, 2025, kupitia akaunti ya Maria Sarungi @MariaSTsehai, alichapisha taarifa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anachezea fedha za Watanzania kwa kumpatia Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Freeman Mbowe, kama namna ya kumwezesha yeye kurudi Ikulu. Alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Januari 10, 2025.