Dodoma. Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), imeandaa kongamano la kusherehekea miaka 48 tangu kuzaliwa kwa CCM huku miongoni mwa mada ikiwa ni mchango wa chama hicho katika kukuza demokrasia nchini.
Akizungumza leo Alhamisi, Januari 30, 2025, Mwenyekiti wa Taifa wa jumuiya hiyo, Fadhili Maganya amesema kuwa kongamano hilo litakalowashirikisha wasomi litafanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center, Februari 2, 2025.
Amesema katika kongamano hilo litajadili chama hicho kilikotoka na kinapokwenda na kutakuwa na wachokoza mada akiwemo mwanazuoni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palagamba Kabudi.
“Sisi tumeanza kama Jumuiya ya Wazazi, watakuja UWT (Umoja wa Wanawake Tanzania) nao watakuwa na siku yao, UVCCM (Jumuiya ya Vijana ya CCM) wana siku yao na kilele kitafanyika tarehe 5, (Februari 5,2025) ambapo mgeni rasmi atakuwa ni mheshimiwa Rais na mwenyekiti wetu wa chama, Rais Samia Suluhu Hassan,”amesema.
Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Ally Hapi amesema mada zitakazowasilishwa mchango wa CCM katika maendeleo ya Taifa, Rais Samia katika kujenga chama cha CCM na Taifa, vijana na elimu katika maendeleo ya Taifa na katika kujenga maadili na malezi, utamaduni, mila na destrori.
“Mada zote zitaongelea miaka 48 ya CCM imefanya nini kwa umma kwa maendeleo ya Taifa,” amesema Hapi.