Rais wa Rwanda, Paul Kagame amemtolea maneno makali, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa akijibu tuhuma alizozitoa rais huyo kwamba Kagame anawasaidia waasi wa M23 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kagame amesisitiza kwamba M23 siyo Wanyarwanda na kumtuhumu Ramaphosa kwamba amepeleka jeshi lake nchini DRC kinyume cha sheria na kwamba anajifanya mpatanishi wakati nyuma ya pazia ana maslahi yake.
Kagame akaendelea ‘kuwaka’ kwamba Ramaphosa hana mamlaka ya kutoa vitisho kwa Rwanda na kwamba wapo tayari muda wowote kujibu chochote wanachotaka kukifanya nchini Rwanda.
Awali, akizungumzia kuhusu kuuawa kwa wanajeshi 13 wa Afrika Kusini waliokuwa nchini DRC, Ramaphosa amenukuliwa akiituhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao na kueleza kuwa nchi yake italipa kisasi.
Kagame ameyasema hayo katika mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya mtandao usiku wa jana na kuhudhuriwa na marais mbalimbali, akiwa Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na William Ruto wa Kenya.
Wengine walioshiriki ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Salva Kiir wa Sudan Kusini, Evarist Ndayishimiye wa Burundi na Dk. Hassan Mohamud wa Somalia.