Kilichomzuia Baleke kutua Namungo chatajwa

MASHABIKI wa klabu ya Namungo walikuwa wakihesabu saa kabla ya kumuona straika wa zamani wa Simba na Yanga, Jean Baleke akitua katika kikosi hicho, lakini imeshindikana na mabosi wa klabu hiyo wameanika sababu zilizomzuia mshambuliaji huyo kujiunga na timu hiyo.

Baleke alijiunga na Yanga katika dirisha kubwa la msimu huu, lakini akashindwa kupata nafasi ya kucheza chini ya makocha Miguel Gamondi na Sead Ramovic na kwenye dirisha dogo ilielezwa amepewa mkono wa kwaheri na alikuwa akijiandaa kutua Namungo kabla ya dirisha hilo kufungwa.

Hata hivyo, Katibu wa Namungo, Ally Seleman amefafanua dili zima la kutaka kumsajili mshambuliaji huyo na kilichokwamisha kutua kwa wauaji hao wa Kusini hadi dirisha lilipofungwa Januari 15.

Seleman alithibitisha ni kweli kulikuwapo mchakato wa kumsajili Baleke, lakini  kilichokwamisha ni mchezaji kutomalizana baadhi ya vitu na klabu, hivyo ikawa ngumu wao kumsajili.

“Baleke kuna mambo ambayo hawakuyaweka sawa na Yanga hivyo haikuwezekana kumsajili na tayari usajili wa dirisha dogo umefungwa, akili zetu kwa sasa tunazieleza kwenye kupambania malengo yetu,” alisema Seleman na kuongeza;

“Baleke ni mchezaji mzuri na bado ni kijana ambaye anahitaji kucheza na kuna usajili wa dirisha kubwa huenda hilo likatokea ama lisitokee akasajiliwa na timu nyingine.”

Licha ya katibu huyo wa Namungo kutoweka wazi, inadaiwa suala la masilahi ni kitu kinachotajwa kuwa sababu ya kushindwa kujiunga na timu hiyo.

Mbali na kiongozi huyo, kocha wa Namungo Juma Mgunda aliwahi kumzungumzia Baleke kwamba bado ni kijana mdogo anapaswa kujifunza jinsi ya kuhimili changamoto ili zisimtoe mchezoni.

“Baleke ni mshambuliaji mzuri, umri wake anahitaji kusaidiwa zaidi kumjenga pia anapaswa kujifunza subra na huwa nazungumza naye mara kwa mara ili asikate tamaa,” alisema Mgunda.

Kwa sasa Baleke amekuwa akionekana akifanya mazoezi binafsi na hivi karibuni alikuwa anacheza na timu za mtaani kwenye Uwanja wa Magunia uliopo Msasani, Dar es Salaam.

Related Posts