Kocha KenGold freshi, BM3 atuliza mashabiki

PAMOJA na kukubali kiwango cha wachezaji, kocha mkuu wa KenGold, Vladslav Heric amesema kazi iliyobaki ni kuongeza makali eneo la ushambuliaji, huku nyota Benard Morrison ‘BM3’ akituliza upepo.

Ken Gold inajiandaa na mzunguko wa pili, ambapo tayari imeshatesti mitambo yake katika michezo miwili ya kirafiki ikiambulia sare ya 1-1 dhidi ya Prisons na Mbeya Combine iliyoisha kwa suluhu juzi.

Kwa sasa timu hiyo ambayo juzi ilitambulisha mastaa wote katika tamasha maalumu, inajiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga, utakaopigwa Februali 5 kwenye Uwanja wa KMC Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwanaspoti, Heric alisema ameangalia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na kuridhishwa na ubora wao, akieleza kuwa tatizo bado lipo kwenye umaliziaji akiahidi kukomaa nao.

Alisema mkakati wake ni kuona timu hiyo inabaki Ligi Kuu licha ya presha iliyopo hivi sasa, akitamba kuwa usajili wa mastaa dirisha dogo, utamaliza kiu ya mashabiki.

“Bado kuna upungufu eneo la ushambuliaji kwa kushindwa kutumia nafasi wanazotengeneza, kwa muda huu kabla ya kushuka uwanjani dhidi ya Yanga, nitatengeneza mkakati mpya,”€ alisema Mserbia huyo.

Kwa upande wake nyota wa timu hiyo, Morrison alisema lengo la wachezaji ni kuona wanaipambania Ken Gold kubaki Ligi Kuu, akieleza kuwa kazi itaanza dhidi ya Yanga kuanza hesabu upya.

Aliwaomba mashabiki kutokata tamaa akieleza kuwa matokeo yaliyopo kwa sasa yanaweza kubadilika na timu kuwa nafasi nzuri kwenye msimamo akisema nia wanayo.

Related Posts