KUTOKA MJENGONI: Kwani Dk Chaya unataka ardhi au fedha?

Dk Chaya, kwani ulitaka wananchi wako warudishiwe hizo ekari 30, au maana ya swali lako nini hasa?

Sema ulisahau kidogo, kwani ungekumbuka kuwa juzi Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, aliwapeni njia ya jinsi mnavyoweza kuwasaidia wapigakura wenu kuhusu ardhi.

Mbunge Dk Pius Chaya alizunguka sana katika swali lake, lakini kumbe alikuwa anajua mahali pa kuweka nondo zake. Haikuwa kitu kingine isipokuwa alitaka kujua kuhusu ardhi ekari zaidi ya 3,000 zilizochukuliwa kutoka kwa wananchi wake kupitia mpango wa uwekezaji.

Serikali haikuficha kitu, badala yake ilimwambia ukweli kuwa wananchi wake wawe wapole wakati inaendelea kulifanyia kazi suala la fidia kwa waliochukuliwa ardhi yao.

Hapo ndipo ujue humu ndani watu wanajichanganya au kusahau! Juzi  Spika Tulia alipigilia msumari kuhusu utwaaji ardhi, akisema hakuna kuchukua kipande cha mtu hadi alipwe fidia.

ZODO USICHOMEKEE MASWALI MAGUMU

Mheshimiwa Mwantumu Zodo, acha kuwazodoa kwa kuchomekea swali juu ya swali! Huoni namna ulivyoichanganya Serikali na uongozi wa Bunge?

Hivi unajua wanapokuja kujibu maswali yenu huwa wamejiandaa na kufanya tafiti ili majibu yao yawe ya uhakika na yenye kutoa matumaini makubwa kwa Watanzania?

Sasa, mbunge huyu jana aliuliza swali la msingi kwa Ofisi ya Rais – Tamisemi, ambalo lilihusu upungufu wa maji kwenye maeneo mengi ya shule za sekondari nchini.

Kicheko kikaja pale alipouliza swali la nyongeza, ambapo aliuliza swali la barabara. Hivi ni vitu viwili tofauti, hata ikampa Naibu Waziri, Zainabu Katimba, kushindwa kujua ajibu nini.

Si huyo tu, bali Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, alisema swali limemchanganya hata yeye, hivyo akamuomba mhusika kuliweka upya.

Ujue hiyo ilitokea baada ya kuwepo kwa utulivu wa dakika kadhaa kati ya Spika na Naibu Waziri, kwani suala la maji linasimamiwa na wizara nyingine tofauti na barabara. Je, kipi kilimsibu au alitaka kutesti mitambo?

KWANI PICHA MNAZOPIGWA KILA SIKU ZINAPELEKWA WAPI?

Leo siwataji, lakini wakati ukifika nitawataja mmoja baada ya mwingine, ikiwemo namba za kamera zinazowapiga picha. Ujue siwaelewi!

Mlioko nje ya viwanja vya mjengo huu, tambueni mpango huu. Baadhi ya wabunge, hasa mama zetu, kila siku wanapoingia bungeni huomba kupigwa picha.

Huwezi kuamini kilichomo ndani ya mjengo, lakini ukweli unabaki hivyo. Mbunge akiingia viwanja vya Bunge, huomba kupigwa picha na kutumiwa kwenye simu yake.

Wabunge hao ni wale shupavu wa kushiriki vikao, si watoro. Jiulize, kwa mpango huu wanakuwa na picha ngapi kwa mwezi? Mbunge akiingia mjengoni hadi apigwe picha akiwa kwenye pozi zuri, hasa akivaa viwalo kisawasawa. Je, picha zinapelekwa wapi?

Nanyi waandishi wa habari mbona mnakuwa hivyo? Yaani mtu mmoja mnamkimbilia kumpiga picha kila siku, mbona wengine hamuwapigi?

WABUNGE HAWA WANAWEZA KUPIMANA UBAVU, WASAIDIENI

Ninyi wabunge mbona mnataka kuvunja meza, wakati jambo lenyewe ni rahisi tu? Mnajenga nyumba moja, acheni kugombania fito.

Niwakumbushe, hata watangulizi wenu katika majimbo yenu walishaanza malumbano hayo muda mrefu, japokuwa hawakufikia mwisho.

Nawazungumzia wabunge Edward Ole Kaita wa Kiteto na Mohamed Monni wa Chemba. Suala la mpaka nusura liwavunjie uheshimiwa wao, sema Spika alituliza.

Monni aliuliza kuhusu mgogoro wa mipaka ya majimbo hayo—moja Dodoma, lingine Manyara, akidai kujua lini utapatiwa ufumbuzi.

Lakini majibu ya Naibu Waziri, Geofrey Pinda, hayakuwafurahisha, wakaamua kusimama na kuanzisha malumbano.

KAGAIGAI UNGEKAA PALEE…

Daa! Dunia inazunguka kweli, na kwa namna yoyote usiishi kwa kukariri kwamba kila siku ni ile ile. Hapana!

Ukisema leo ni Jumatatu, inabidi utambue kuwa zipo siku nyingine kama Jumanne, Alhamisi na nyinginezo ndani ya wiki.

Ukitaka kujua hilo, angalia jinsi ilivyokuwa jana pale alipoingia mjengoni mtu aliyewahi kuwa maarufu, anayezijua kona na vyumba vyote vya mjengo, na kwa kweli huwezi kumtisha.

Huyu ni aliyewahi kuwa Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai, kabla ya kupewa majukumu mengine ya ukuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, kisha kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Utangazaji Tanzania.

Usingeamini kuwa mwamba anaweza kuwekwa kwenye viti vya wageni, lakini ndivyo ilivyokuwa jana, na wabunge walimpigia makofi ya kutosha wakimpa heshima yake kama mtu waliyedumu naye hapo.

Kagaigai, hapana shaka ulikuwa ukijua kila kitu kilichofanyika jana. Je, hujamisi mjengoni, hasa kwenye ratiba zako za kudamka alfajiri kukagua ukumbi? Sema taratibu basi!

Yaliyoandikwa sio maneno halisi waliyozungumza au kuongea wabunge, ni utani tu

Related Posts