Bunda. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Steven Wasira amesema wale wote wanaosema chama hicho kimekaa muda mrefu madarakani wanapaswa kufahamu kuwa hakikuwa na mkataba wa kumaliza kazi, isipokuwa kuleta maendeleo kwa wananchi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Bunda leo Jumatano, Januari 30 2025, Wasira amesema chama hicho hakina mpango wa kutoka madarakani kwani kazi ya kuleta maendeleo bado inaendelea ingawa imekwishafanyika kwa kiasi kikubwa.
“Eti kuna mtu anauliza mnaonaodoka lini, eti mmekaa sana madarakani, hatuondoki ng’o, kazi bado inaendelea,” amesema Wasira.
Amesema Chama cha Mapinduzi ambacho ni matokeo ya mungano wa vyama vya Tanu na ASP kilipewa jukumu la kuleta ukombozi kwa wananchi sambamba na kuleta maendeleo na kwamba kazi ya kueleta maendeleo ni kazi endelavu hivyo yeyote mwenye ndoto za chama hicho kuacha kushika dola anajisumbua.
Wasira amesema baada ya Rais wa awamu ya tano, Dk John Magufuli kufariki dunia hofu kubwa ilitanda miongoni mwa wananchi wakihofia utekelezaji wa miradi mikubwa aliyoinzisha Dk magufuli lakinin hivi sasa hofu hiyo imetoweka kwani miradi yote imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
“Kuna Bwawa la Nyerere ambalo utekelezaji wake unaendelea na upo katika hatua nzuri kuna Daraja la Magufuli pale Busisi nimepita jana utekelezaji wake umefika zaidi ya asilimia 90, kuna reli ya umeme hivi sasa infanyakazi kiasi kwamba wale wote waliokuwa wanasema makao makuu ya nchi ni mbali sasa hivi ni mwendo wa masaa matatu tu umefika,” amesema.
Wasira amesema katika kipindi cha miaka minne, Rais Samia amefanya mambo mengi makubwa kwaajili ya wananchi na kwamba hayo yote yanatekelezwa kutokana na ukweli kuwa kazi ya CCM ni kuwatetea wananchi pamoja na kuwaletea maendeleo.
Amesema ili kuleta mshikamano wa kitaifa Rais Samia alipoingia madarakani alitaka kuwepo kwa maridhiano na kwamba pamoja na nia hiyo lakini suala la amani na utawala bora ni lazima kufuatwa.
“Wakati wa kutekeleza zile R4 za Rais wenzetu walikuja na mambo mengi ambayo Rais alitekeleza baadaye wakaja na suala la wale wabunge 19 eti waondolewe bungeni tukawaambia hilo suala liko mahakamani, wakaja na jambo jingine eti tujifungie tutengeneze katiba tukawakatalia kwasababu suala la katiba ni la wananchi sasa tulivyowakatalia wakaamua kujiondoa kwenye maridhiano,” amesema.
Amewaomba wananchi kukipigia kura chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa maelezo kuwa sambamba na mambo mengine suala la amani ya nchi ni jukumu kuu la CCM huku akisema hakuna chama chenye uwezo wa kufanya hivyo kama ambabyo chama chake kimefanya kwa miaka 60 sasa.
Amesema anashangaa watu wanaohoji kazi iliyofanywa na CCM katika kipindi cha miaka 60 iliyopita na kwamba wote wanaohoji wameamua kufanya hivyo huku ukweli wakiwa wanaujua kwani yapo mengi yaliyofanyika katika kipindi hicho.
“Kipindi tunapata uhuru tulikuwa na barabara tatu tu ambazo zilikuwa zinatumiwa na wazungu kwenda kwenye mashamba ya mikonge na kahawa kutoka Dar kwenda Morogoro, kutoka Tanga kwenda Korogwe na kutoka Moshi kwenda Arusha lakini hivi sasa serikali ya CCM imeunganisha nchi nzima kwa barabara za lami, leo unaweza kutoka hapa hadi Mtwara kwa bajaji,” amesema Wasira.
Amesema serikali imefanya mambo mengi ya kimaendeleo katika kipindi hicho na kwamba upo utofuati mkubwa wa hali halisi ya mandeloe kwasasa ikilinganisha na wakati wa uhuru.
Wasira pia ameagiza kushughulikiwa kwa dosari zilizojitokeza kwenye malipo ya fidia katika eneo la Nyatwali ili kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake kwani chama hicho hakiko tayari kuona mwananchi yeyote anaonewa.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Bunda Mjini, Robert Maboto amesema Serikali imefanya mambo mengi na mabadiliko yanaonkena na kwamba kazi bado zinaendelea huku akitolea mfano wa malipo ya fidia kwa wanachi wa Kata ya Nyatwali ambao wamelipwa zaidi ya Sh49 bilioni ili kupisha shughuli za uhifadhi.
“Suala la maji ilikuwa ni changamoto kubwa lakini leo maji yanapatikana kwa kiasi kikubwa isipokuwa kata za pembezoni bado kuna changamoto lakini ipo miradi mikubwa inaendelea, suala la shule za sekondari na Msingi serikali imefanya mambo mengi na kazi bado zinaendelea,” amesema Maboto.
Amesema hivi sasa wananchi wa Bunda mjini wanasubiri utekelezaji wa miradi kadhaa ikiwepo ujenzi wa soko jipya na stendi ya kisasa ili hatua ambayo itasaidia kuimarisha uchumi wao.