Mapendekezo, matumaini uhakika ARV | Mwananchi

Dar es Salaam. Licha ya uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump kusitisha misaada ya maendeleo nje ya nchi hiyo kuwa tishio kwa upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV) bila malipo, wadau wameonesha matumaini ya kuendelea kupatikana kwa dawa hizo.

Matumaini ya wadau hao yanatokana na kile walichoeleza, si Marekani pekee aliyekuwa anatoa msaada wa dawa hizo, Global Fund na washirika wengine ndani ya Shirika la Afrika Duniani (WHO) walikuwa wanatoa.

Kama hatua za kuukabili utegemezi wa misaada nchini, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha ACT-Wazalendo wameshauri kuwapo na mipango ya dharura ya kisera na kibajeti kugharimia dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi.

Maoni ya wadau hao, yamekuja siku chache tangu Trump atangaze kusitisha misaada hiyo na kuondoa ufadhili wa Marekani ndani ya WHO, hatua zinazohofiwa kuhatarisha ustawi wa baadhi ya mataifa yaliyokuwa yakitegemea misaada hiyo.

Uamuzi wa kusitishwa kwa misaada hiyo umeenda sambamba na tamko la kusitisha hata miradi iliyokuwa inaendelea kufadhiliwa na nchi hiyo.
 

Jana, akizungumza na Mwananchi, Mshauri wa Masuala ya Afya, Dk Elisha Osati alisema ingawa hatua ya Trump inaibua wasiwasi kwa mataifa yaliyokuwa yanategemea misaada, upande wa ARV Tanzania pengine isiathirike, kwani Marekani siyo pekee iliyokuwa inaisaidia Tanzania dawa za ARV. “Kikubwa ARV hazitoki Marekani tu, zinatolewa pia na Global Fund ambayo pia inatoa fedha za kifua kikuu na malaria na washirika wengine wa WHO, hiyo ndiyo inayotupa matumaini,” alisema.

Alisema hatua hiyo haitaiathiri Afrika pekee, bali na mashirika yasiyo ya kiserikali ya Marekani yanayojiendesha kwa kusaidia programu za afya Afrika. “Lakini naona kwa sasa majaji wa Marekani wameonyesha nia ya kusitisha kwa muda katazo hilo ili kutoa nafasi ya majadiliano,” alisema.
 

Kupitia taarifa ya Chadema iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Afya na Maendeleo ya Jamii ya Bunge la Wananchi, Ashura Masoud alisema Serikali inapaswa kuandaa mkakati wa dharura wa kisera na kibajeti ili iwe na fedha za kutosha kwenye mfuko wa kudhibiti Ukimwi.

Alisema Bunge linapaswa kulijadili jambo hilo kwa dharura na Serikali iwasilishe bungeni taarifa ya tathimini na mkakati wa kina wa namna ya kukabiliana na upungufu wa fedha katika sekta zote.
“Rais ashauriane na wakuu wenzake wa nchi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Afrika (AU) wafanye mkutano wa kutafuta ufumbuzi,” ilieleza taarifa hiyo.

Alidai kuwa idadi ya waathirika wa VVU hadi sasa wanaofaidika na misaada ya dawa za kufubaza VVU ni takriban milioni 1.5 na wastani wa Sh204 bilioni kwa mwezi mmoja hutumika, hivyo sitisho la Marekani litaathiri huduma ya ARV na mapambano ya VVU kwa zaidi ya asilimia 50.

Ashura kupitia taarifa hiyo, alimnukuu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Dare, Dk Lilian aliyeitaka Tanzania kujiandaa vilivyo, kwani uwezo wa kuchangia ARV, VVU na Ukimwi ni asilimia sita pekee kupitia bajeti ya Wizara ya Afya na Mfuko wa Udhamini wa Ukimwi (ATF).

Waziri Kivuli wa Afya wa ACT- Wazalendo, Dk Elizabeth Sanga aliitaka Serikali ipunguze matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza fedha kwenye huduma za afya.
Alipendekeza kuanzishwe mfuko wa huduma za afya ya kitaifa kwa kutumia rasilimali za ndani kama madini na utalii kufadhili mfumo wa afya unaojitegemea.

“Serikali iongeze bajeti ya afya kutoka wastani wa asilimia 5.7 hadi kufikia asilimia 10 ya bajeti kuu 2025/2026, ili kupunguza utegemezi na kuboresha huduma za afya,” alisema.
Aliitaka Serikali iharakishe utekelezaji wa mfumo wa kuwaunganisha Watanzania na Hifadhi ya Jamii na kutoa bima ya afya kwa wote ili kuongeza uwezo wake kugharamia, na kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya bila ubaguzi wa kifedha.

Related Posts