Mapya yaibuka Soko la Kariakoo, Samia ang’aka

Dar es Salaam. Wakati Soko la Kimataifa la Kariakoo jijini Dar es Salaam likitarajia kuanza tena kutoa huduma, Rais Samia Suluhu Hassan amesema moto ulioliteketeza, ulikuwa ni kupoteza ushahidi kutokana na ufujaji wa fedha.

Mbali na hilo, amebainisha ukwepaji kodi unaofanywa na wafanyabiashara akitolea mfano walichobaini kwenye jengo la ghorofa lililoporomoka Novemba 16, 2024 Kariakoo  na namna  mizigo inavyohifadhiwa kinyemela kwenye majengo mengi.

Rais Samia amesema hayo leo Alhamisi, Januari 30, 2025, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya chakula cha mchana alichokiandaa pamoja na washiriki wa shughuli ya uokoaji wa kuporomoka kwa jengo hilo.

Katika tukio hilo, watu 31 walipoteza maisha, zaidi ya 80 wakijeruhiwa huku mali na miundombinu ikiharibika na kupotea.

Soko la Kimataifa la Kariakoo, liliteketea Julai 10, 2021 na kuteketeza mali za wafanyabiashara zilizokuwa sokoni humo kisha Serikali ikatoa Sh28 bilioni kwa ajili ya kulikarabati, shughuli iliyoanza tangu Januari 2022.

Ukarabati huo pia, ulikwenda sambamba na ujenzi mpya wa soko dogo litakalokuwa na ghorofa sita kwenda juu na mbili kwenda chini kusaidia shughuli za kibiashara kufanyika kwa ufanisi.

Katika kipindi hicho cha ujenzi wafanyabiashara waliokuwepo sokoni hapo, walihamishiwa kwa muda katika masoko ya Kisutu, Machinga Complex na Karume.

Msingi wa maelezo hayo ya Rais Samia yametokana na ombi lililowasilishwa kwake na  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Severine Mushi kwenye hafla hiyo ya chakula cha mchana, alipokuwa akitoa salamu za wafanyabiashara wa Kariakoo.

Pamoja na mambo mengine, Mushi amemkaribisha kutembelea wafanyabiashara hao,  kwa kile alichoeleza hakuwahi kuwatembelea kabla ya ajali hiyo ya kuporomoka jengo ambapo alikwenda kuwapa pole.

“Mama wafanyabiashara wa Kariakoo wamekumisi, wanatamani uwatembelee, uzungumze nao maana tangu umeingia madarakani (Machi 19, 2021) ulitutembelea wakati wa janga la kuporomoka jengo na tunashukuru kwa hilo ila tunakukaribisha tena wakati mwingine utakapokuwa na nafasi uje ututembelee,” amesema Mushi.

Akijibu hilo Rais Samia amesema:“Kuhusu kuja Kariakoo labda nikukumbushe, nilikuja na siku mbili baada ya mimi kuondoka soko mkalitia moto, sababu za kufanya hivyo nilisema changamoto za uongozi wa mambo yaliyokuwa yanaendelea ndani ya soko na niliagiza vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi sasa ili kupoteza ushahidi mkaamua kulitia moto.”

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha mchana pamoja na washiriki wa zoezi la uokoaji wa ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa eneo la Kariakoo leo  Januari 30, 2025 Ikulu jijini Dar es Salaam

Ziara sokoni hapo anayoizungumzia Rais Samia aliifanya Juni 1, 2021 na siku hiyo alionesha kutoridhishwa na uendeshwaji wa soko hilo, huku akielekeza kufanyika kwa tathmini pamoja na kusimamishwa uongozi wa soko wakati vyombo vya usalama vikifanya uchunguzi.

“Serikali lengo lake ni kusaidia wafanyabiashara wadogo wadogo lakini niliyoyaona hapa naona kama usaidizi wa wafanyabiashara wadogowadogo haupo, ila kuna kutengeneza faida kwa uongozi wa soko au shirika.

Mipango ya uingizaji bidhaa haimpi unafuu mfanyabiashara mdogo, kwa maana hiyo uamuzi wangu ni kwamba tutafanya tathmini ya uendeshaji wa soko na tuone kama hili soko liendelee kusimamiwa na uongozi uliopo au jiji lichukue.”

“Wakati tunafanya tathmini niagize kusimamishwa kwa uongozi wa soko na tuvitake vyombo vya Serikali vifanye uchunguzi halafu tutakuja kutoa uamuzi lakini kwa ujumla hali ya hapa haijaniridhisha na tunakwenda kuchukua hatua zinazofaa ila endeleeni na biashara Serikali iko pamoja nanyi,” alisema Rais Samia akiwa sokoni hapo.

Siku 39 baada ya ziara hiyo, usiku wa Julai 10, 2021 moto ulizuka kuanzia katika eneo la paa  la soko hilo na baadaye kuendelea kusambaa katika maeneo mengine na kuteketeza mali za wafanyabiashara.

Baada ya tukio hilo, Serikali ilitoa Sh28 bilioni kwa ajili ya kulikarabati, shughuli ambayo ilianza Januari 2022.

Jana Jumatano, Januari 29, 2025, Mwenyekiti wa Kamati ya Bodi ya Shirika la Masoko, Hawa Ghasia akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alisema soko hilo liko tayari kwa matumizi kuanzia Februari.

Ghasia alisema baada ya uhakiki wa majina, wafanyabiashara wenye sifa ya kurejea ni 1,520, ikiwa ni ongezeko la wafanyabiashara 601 waliofanyiwa uhakiki mara ya kwanza.

Kuhusu ukwepaji kodi, Rais Samia amesema uamuzi wa Serikali kulijenga soko hilo ni kuwezesha biashara kurejea katika hali ya kawaida, huku akiwasisitiza wafanyabiashara kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha biashara zinakuwa na tija kwa Taifa.

“Naomba wafanyabiashara na Serikali tushirikiane katika maeneno yote, miundombinu, uendeshaji na ulipaji wa kodi. Tusipolipa kodi itakuwa hasara kubwa kwa Taifa. Wafanyabiashara wengi wadogo na wa kati wanakwepa kulipa kodi, tukifanya hivyo nchi yetu inakuwa ombaomba.”

“Pia tutapunguza nchi yetu kuingia kwenye mikopo maana tunakopa kujenga na kutengeneza nchi halafu bado watu wanasema Serikali yetu inaongoza kwa kukopa. Tunakopa kukuza hadhi ya nchi yetu, hakuna anayependa kukopa, ikiwa kila mfanyabiashara atalipa kodi kiwango cha kukopa kitapungua.

Akitolea mfano wa kilichotokea kwenye jengo lililoporomoka la Kariakoo,  amesema ajali hiyo imewezesha Serikali kubaini mchezo mchafu wa wafanyabiashara wa kurundika shehena ya mizigo katika majengo, ambayo hayana uwezo jambo ambalo linahatarisha usalama wa watu na mali.

“Somo lingine nililoliona kwa haraka haraka na pengine ndilo kwa wakati ule lilileta mzozo kwa wafanyabiashara wa Kariakoo, ni mali inayofichwa mle ndani na pengine bila kulipiwa kodi.

“Kuporomoka kwa jengo lile kumetufunulia mambo, sidhani kama zile tani 800 zilizokutwa mle zililipiwa kodi na ndiyo ulikuwa ugomvi mkubwa wa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) kupeleka watu kuangalia maghala ndani ya eneo la Kariakoo,” amesema.

Katika taarifa yake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema licha ya jengo hilo kuwa na uwezo wa kuhifadhi mzigo wa tani 250 mzigo halisi uliokutwa ni tani 850.

Pamoja na kuwaokoa watu 71 uchambuzi wa mizigo ulifanyika na tulifanikiwa kupata robota 2044 na viroba 10,051 vyenye uzito wa tani 850 vilikuwa kwenye jengo hilo, jengo hilo lilikuwa na uwezo wa kubeba tani 250 tu.

“Pia tulipata fedha taslimu Sh112.8 milioni, dola za Marekani 48,490, Shilingi za Kenya 6920, fedha za China Yuan 631. Mali hizo na fedha zote zimeendelea kurejeshwa kwa wamiliki waliotambuliwa.

Kamati ya uchunguzi wa tukio la kuporomoka kwa jengo na kufanya uchunguzi wa kina wa majengo mengine yaliyopo Kariakoo, imehitimisha kazi yake na taarifa imeshawasilishwa ofisi ya waziri mkuu tutaiwasilisha kwako Rais utakapokuwa tayari,” amesema Majaliwa.

Akizungumzia hilo, Rais Samia amesema kitendo hicho kimeifanya Serikali kubaini kukosekana kwa usimamizi wakati wa ujenzi na kuhakikisha viwango vya ujenzi vinafuatwa hali inayosababisha ukiukwaji wa taratibu.

“Tumepata somo la jinsi biashara inavyoendeshwa pale Kariakoo, kama jengo lina uwezo wa kuchukua mzigo  tani 250 lakini zimekutwa tani 800 hivyo kwa vyovyote vile lisingeweza kubeba. Hilo ni jengo moja ila nina uhakika majengo yote yako vilevile.

“Upanuzi wa majengo na uongezaji wa nafasi unafanywa kwa msingi ule ule wa awali na si kuanza tena. Kinachofanyika ni kurefusha juu na kuchimba chini.

Katika hili tumejipanga kuanzia sasa tutahakikisha viwango vya ubora vya ujenzi vinazingatiwa ipasavyo na taratibu za ukaguzi wa majengo zinaimarishwa, sheria za ujenzi zinafuatwa na rasilimali za kiufundi zinapatikana kwa ajili ya kusimamia sekta hiyo muhimu.

Alichosema Rais Samia kinashabihiana na ripoti zilizowahi kuandikwa kuhusu kuporomoka kwa majengo, ambapo ukiukwaji wa viwango vya msingi wa jengo na mabadiliko ya matumizi ya jengo husika ni baadhi ya sababu za kuanguka kwa majengo hayo.

Mwaka 2006 jengo liliporomoka eneo la Chang’ombe, Dar es Salaam na kuua watu wanne. Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa alitoa maagizo watu wawajibishwe kwa uzembe uliojitokeza.

Juni 21, 2008 ghorofa jipya lililokuwa linajengwa mitaa ya Mtendeni na Kisutu lilianguka na kuangukia jengo dogo walimokuwa wakiishi watu.

Machi 29, 2013 jengo la ghorofa 16 katika makutano ya barabara za Zanaki na Indira Ghandi lilianguka na kusababisha vifo vya watu 36, sababu ya kuporomoka ikitajwa kuwa ujenzi usiozingatia utaalamu.

Kutokana na matukio hayo, kampuni ya Design Plus Architects (DPA) ilipewa zabuni ya kukagua majengo Manispaa ya Ilala kuona usalama wake na Novemba 5, 2013, ilitoa ripoti kuwa kati ya maghorofa 90 yaliyokaguliwa, 67 yalikuwa yalijengwa kinyume cha sheria. Kampuni hiyo ilisema baadhi ya majengo hayo yanaweza kuporomoka kutokana na ujenzi wake kuwa chini ya kiwango.

Nje ya Dar es Salaam, Desemba 19, 2022 watu watano walifariki dunia na wengine tisa walijaruhiwa baada ya kuangukiwa na jengo la ghorofa mbili lililokuwa linaendelea kujengwa, katika Kijiji cha Sembeti, Marangu mkoani Kilimanjaro. Kulikuwa na mafundi na vibarua wapatao 30.

 Kwa upande wa Zanzibar Januari 25, 2017 jengo moja katika Mtaa wa Hurumzi, Unguja lilianguka wakati mafundi wakilifanyia ukarabati.

Eneo lingine alilozungumzia Rais Samia ni kukosekana kwa ushindani wa kibiashara kati ya wafanyabiashara wazawa na wale wanaotoka nje ya nchi kilio kilichowasilishwa na Mushi.

Mushi amesema kwa sasa wanakabiliana na ushindani mkubwa na wafanyabiashara wa kigeni hali inayotishia ustawi wa biashara za wazawa katika eneo hilo la Kariakoo.

Akijibu hilo Rais Samia alisema:“Nimeelekeza TRA kutopendelea wafanyabiashara wote walipe kodi na wawe na usawa katika soko.”

Pia akamuelekeza Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Seleman Jaffo kuangalia vyema suala la wageni kufanya biashara zinavyofanywa na wenyeji.

“Waziri wa biashara naomba ukaliangalie vyema suala la wageni kufanya biashara zinazofanywa na wenyeji, niliwahi kurushiwa clip ya Kariakoo mgeni anapigana na wenyeji nikauliza kwanini wanapigana wakasema yule ni mmachinga. Haiwezekani mgeni akawa mmachinga je vijana wetu watafanya shughuli gani?” amehoji.

Rais Samia amesema kuporomoka kwa jengo la Kariakoo kumeacha somo la umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa,  na kuhakikisha nchi inakuwa na utayari wa kukabiliana na dharura wakati wowote.

“Mpango wetu wa baadaye ni kuhakikisha tunakuwa na vifaa, rasilimali na utaalamu unaohitajika ili kukabiliana na majanga kwa haraka na ufanisi zaidi. Sekta binafsi ilijitoa kwa vifaa vyenye uwezo wa hali ya juu ambavyo tulipaswa kuwa navyo na sisi upande wa Serikali.

Tunakwenda kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa ikiwemo tahadhari ya mapema, kuzijengea uwezo timu na kamati za usimamizi wa maafa katika ngazi ya mikoa na wilaya,” amesema Rais Samia.

Unaweza kusema ni zimwi la matukio mbalimbali linaiandama Kariakoo ikiwa ni baada ya jengo lililopo sokoni hapo linalotumiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwaka moto leo saa 6 mchana.

Jengo hilo lenye sakafu tano, ni moja pekee ndiyo imeteketea kwa moto huku watumishi wakitoka salama baada ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufanikiwa kudhibiti moto huo.

Baada ya taarifa za moto huo kusambaa, jitihada mbalimbali za kuudhibiti zilianza kufanyika na baadhi ya wafanyabiashara waliokuwapo eneo hilo,  kabla ya dakika chache baadaye magari ya zimamoto kufika.

Hadi saa 7 mchana Mwananchi ilipofika maeneo hayo ilikuta magari sita ya zimamoto yakiwa yameegeshwa huku kifaa cha kisasa kinachowezesha uzimaji moto katika majengo marefu kikisogezwa karibu na jengo hilo.

Magari ya zimamoto yaliendelea kupishana kadri kila moja lilipokuwa likimaliza maji na kuondoka.

Alipozungumzia shughuli hiyo, Naibu kamishana wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Goodluck Zelotha amesema wamefanikiwa kuudhibuti moto kwa asilimia 98.

“Tulipopata taarifa tulichukua mitambo inayowezesha uzimaji moto kwenye majengo marefu na magari kuja eneo hili na zoezi lilianza mara moja,” amesema Goodluck na kuongeza

“Mpaka sasa operesheni inaendelea na itakapokamilika tutatoa taarifa ya jumla.

Wakati yeye akiyasema hayo, Kamishna wa TRA, Yusuph Mwenda amesema watumishi wote waliokuwapo ndani ya jengo hilo wako salama.

“Kwa upande wa madhara ya mali hatujafanya tathmini lakini ni ghorofa ya tano ambayo imeteketea, Niwashukuru Zimamoto kwa kuja na vifaa na wamekuwa na uwezo wa kuzima kwa haraka,” amesema Mwenda.

Kwa upande wa uharibifu uliotokea amesena watafanya tathmini ya haraka ili walipa kodi wasishindwe kupata huduma ambazo walitakiwa kupata.

“Tathmini zitaonyesha chanzo ni nini na tutachukua hatua za haraka ili kuzuia jambo hili lisitokee tena,  lakini niwahakikishie tu rekodi za walipa kodi hazikai sakafu ya tano zinakaa sehemu nyingine hivyo ziko salama,” amesema.

Related Posts