Miili 18 yaopolewa ajali ya ndege, helikopta Marekani

Washington. Televisheni ya CBS News imeripoti kuwa tayari miili ya watu 18 imeopolewa kutoka kwenye maji ya mto ambao ajali ya ndege ya abiria ya Shirika la Ndege la Marekani (American Airlines) iliyogongana na Helkopta ya Jeshi la nchi hiyo aina ya UH-60 ‘Black Hawk’.

Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia leo Alhamisi Januari 30, 2025 katika uwanja wa ndege wa kitaifa wa Reagan wakati ndege hiyo ikienda kutua katika uwanja huo jijini Washington DC.

Ndege hiyo ya abiria ya Shirika la Ndege la Marekani namba 5342 ilikuwa na abiria 60 na wahudumu wanne huku helkopta ya kijeshi ikiwa na wanajeshi watatu waliokuwa kwenye mafunzo.

Kwa mujibu wa CBS News, tayari maofisa wa dharura na uokozi zaidi ya 300 wamewasili ulipo Mto Potomac uliopo karibu na Ikulu ya Washington nchini humo ambapo ndipo ndege hizo zimeanguka baada ya kugongana.

Vyombo vingine vya habari ikiwemo the Washington Post, vimeripoti kuwa hadi sasa hakuna manusura aliyepatika katika jitihada za uokoaji zinazofanywa na maofisa zaidi ya 300 walioko eneo hilo. Hata hivyo, imedai kushuhudia miili ya watu ikitolewa majini.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege la Marekani, Robert Isom ametoa taarifa kwa Umma akisema: “Sasa hivi tumejikita kuangalia usalama wa abiria waliokuwemo, wahudumu na familia zao, tunaendelea kuwasiliana na mamlaka husika kuhusiana na suala hili sambamba na kutoa huduma za dharura.”

Kufuatia ajali hiyo, Rais Donald Trump ameeleza kukasirishwa nayo huku akisema ajali hiyo ingeweza kuepukika huku akiwanyooshea kidole wasimamizi wa uwanja wa ndege ilipotakiwa kutua ndege hiyo.

“Ajali hii ingeweza kuzuilika. Kwa nini wafanyakazi waliokuwa kwenye mnara wa kuongozea ndege wasingewaambia wanajeshi waliokuwa ndani ya helkopta mbinu mbadala ya kufanya baada ya kuona ndege hiyo ikielekea kutua. Mazingira ya ajali hiii yanaonekana wazi kuwa ingeweza kuzuilika,” amesisitiza Trump.

Trump ameandika ujumbe huo kwenye akaunti ya mtandao wake wa Truth Social huku akisisitiza kuwa hajafurahishwa hata kidogo na mazingira ya ajali hiyo.

Meya wa Alexandria, Alyia Gaskins ameielezea ajali hiyo kuwa anachokiona eneo la ajali kinatisha.

“Tulishtushwa baada ya kusikia kuna ndege zimegongana hapa,” amesema Meya huyo huku akiomba maombi yaongezwe kwa waathiriwa wa ajali hiyo.

Seneta wa Jimbo la Kansas nchini humo, Roger Marshall amesema kinapotokea kifo cha mtu yoyote ni huzuni kwao, hata hivyo, vinapotokea vifo vingi kwa wakati mmoja hilo ni janga kwa taifa.

Seneta huyo ameshindwa kuelezea hali ya ndege hizo ambazo zimegongana huku akidokeza kuwa taarifa kamili itatolewa baada ya shughuli ya uokoaji na unasuaji wa waliofariki itakapokamilika.

Alipoulizwa iwapo kuna manusura yoyote, Mkuu wa Idara ya Zimamoto katika eneo hilo, John A. Donnelly amesema: “Bado hatujafahamu kama tutafanikiwa lakini tunaendeleza jitihada za kufanikisha hilo.”

Helkopta aina ‘Sikorsky UH-60 Black Hawk’ iliyogongana na ndege hiyo ya abiria ni miongoni mwa helkopta chache zinazotajwa kuaminika kwenye operesheni za kijeshi za Jeshi la Marekani.

Helkopta hiyo ni moja kati ya helkopta za kijeshi 5,000 zilizotengenezwa nchini humo tangu miaka ya 1970, zilitumiwa kwenye operesheni za kijeshi maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika

Related Posts

en English sw Swahili