Dar es Salaam. Wizara ya Afya Uganda, imethibitisha mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Ebola, ‘Sudan Ebola Virus Disease’ (SVD) jijini Kampala baada ya sampuli kuthibitishwa na maabara tatu za kitaifa.
Taarifa hiyo iliyotolewa leo Alhamisi, Januari 30, 2025 imeelezea kuwa tukio la kwanza, muuguzi mwenye miaka 32 kutoka Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Mulago, alifariki dunia baada ya kuonyesha dalili kali za ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo marehemu, ambaye alikuwa akifanya kazi katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Mulago, alianza kuonyesha dalili kama za homa na alitafuta matibabu katika vituo kadhaa vya afya, ikiwa ni pamoja na Mulago, Hospitali ya Saidina Abubakar Islamic huko Matugga na Hospitali ya Rufaa ya Mbale jijini Mbale.
Hali yake ilizidi kuwa mbaya, akianza kutoka damu katika sehemu mbalimbali za mwili, kushindwa kufanya kazi kwa viungo muhimu vya mwili na hatimaye kufariki jana Januari 29, 2025.
Uchunguzi wa baada ya kifo ulithibitisha uwepo wa virusi vya Sudan Ebola.
Kufuatia hilo, Wizara ya Afya ya Uganda imesema imechukua hatua za haraka kudhibiti mlipuko huo.
“Kikosi cha usimamizi wa dharura kimeanzishwa. Timu za haraka za kukabiliana na dharura zimetumwa Mbale na Matugga ili kufuatilia na kudhibiti hali hiyo. “Ufuatiliaji wa waliokutana na mgonjwa unaendelea,” imeeleza taarifa hiyo.
Imesema jumla ya watu 44 waliokutana na mgonjwa wametambuliwa, wakiwemo wahudumu wa afya 30 na wagonjwa kutoka Mulago, wanafamilia 11 wa marehemu na wahudumu wa afya wanne kutoka Hospitali ya Saidina Abubakar Islamic.
Ugonjwa wa Ebola umeendelea kuwa tishio Afrika Mashariki, huku Uganda ikishuhudia milipuko kadhaa katika miaka ya nyuma. Aina ya Sudan Ebola Virus inatofautiana na aina ya Zaire, ikiwa na kiwango cha juu cha vifo na kwa sasa haina chanjo iliyoidhinishwa.
Mlipuko wa hivi karibuni nchini Uganda ulitokea mwaka wa 2022, na kusababisha hatua kubwa za afya ya umma kuchukuliwa.
Ebola ni ugonjwa mbaya unaosababishwa na virusi kutoka familia ya Filoviridae. Huenea kupitia mgusano wa moja kwa moja na majimaji ya mwili ya mtu aliyeambukizwa, nyuso zilizochafuliwa, au wanyama waliombukizwa.
Maumivu makali ya kichwa
Maumivu ya misuli na udhaifu
Kutapika na kuhara
Kutokwa na damu au mabaka yasiyoeleweka
Kushindwa kufanya kazi kwa viungo muhimu vya mwili katika hali mbaya
Kwa sasa hakuna chanjo iliyoidhinishwa kwa aina ya Sudan ya Ebola, ingawa chanjo kama Ervebo (rVSV-ZEBOV) imeonyesha mafanikio dhidi ya aina ya Zaire. Matibabu yanajikita zaidi katika huduma za uangalizi, zikiwemo: Kutoa maji mwilini na kurekebisha usawa wa electrolytes
Kurekebisha shinikizo la damu
Matibabu ya majaribio kwa kutumia kingamwili za monoclonal
Kuepuka mgusano wa moja kwa moja na watu walioambukizwa
Kudumisha usafi wa mikono na kutumia vifaa vya kujikinga (PPE)
Kuhakikisha mazishi salama kwa watu waliofariki kutokana na Ebola
Kampeni za uhamasishaji wa umma ili kudhibiti mlipuko.