Muswada uwekezaji wa umma mbioni kupelekwa bungeni, Diaspora watajwa

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema uundwaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma unasubiri kupitishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Alhamisi Januari 30, 2025 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo.

Nyongo ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), Dk Pius Chaya (CCM) ambaye ameuliza lini Serikali itaunda Mamlaka ya Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma ili kuimarisha usimamizi wa uwekezaji ndani ya Serikali.

Katika swali la nyongeza mbunge huyo amehoji pia kuhusu suala ardhi kubwa ya wananchi wa Manyoni ambayo ilichukuliwa kwa mtindo wa uwekezaji akitaka kujua hatima yao kama uwekezaji haufanyiki.

Naibu Waziri amesema kwa sasa muswada wa Sheria hiyo, umesomwa kwa mara ya kwanza mwezi Novemba, 2023 na kuelekezwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kwa ajili ya uchambuzi.

“Mara baada ya kamati kukamilisha kazi hiyo, muswada huo utapelekwa bungeni kwa ajili hatua zingine zinazofuata za utungwaji wa sheria, hivyo mheshimiwa mbunge aendelee kuvuta subira,” amesema Nyongo.

Kuhusu ardhi ya wananchi wa Manyoni iliyochukuliwa, amesema Serikali inaendelea kulifanyia kazi eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 3,000 na mara mipango itakapokuwa tayari wananchi waliochukuliwa maeneo hayo watalipwa.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri amesema miongoni mwa mambo yanayotazamwa ni pamoja na suala la diaspora ambao nao wanapaswa kuingizwa kwenye mpango huo ili kuweka uwiano.

Akijibu kuhusu viwango vya thamani ya uwekezaji, amesema kwa mgeni sheria inamtaka mgeni kuwa na uwekezaji unaozidi Dola 200,000 wakati kiwango cha uwekezaji kwa wazawa ni dolla zisizopungua 50,000 huku suala la Diaspora likitaraji kujadiriwa ili kuwapa unafuu.

Related Posts