Mgogoro unaoendelea katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umeendelea kuibua mvutano mkubwa kati ya viongozi wa Afrika, hususan Rais Paul Kagame wa Rwanda na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.
Matamshi yao makali na shutuma wanazotoa waziwazi zimeweka bayana msuguano mkubwa kati ya mataifa haya mawili yenye ushawishi barani Afrika.
Katika siku za hivi karibuni, mapigano kati ya kundi la waasi la M23 na Jeshi la DRC (FARDC) yameongezeka kwa kiwango cha kutisha na kuhusisha majeshi ya SADC Mission in the Democratic Republic of Congo (SAMIDRC), ambako wanajeshi wa Afrika Kusini, Tanzania na Malawi wanashiriki.
Tukio hili limeongeza mvutano wa kidiplomasia huku viongozi wa mataifa mbalimbali wakitoa kauli zinazofichua mgawanyiko wa kimtazamo kuhusu mgogoro huu.
Matamshi ya Rais Ramaphosa
Akizungumzia hali ya sasa, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, alielezea masikitiko yake kutokana wanajeshi wa Afrika Kusini waliokuwa wakihudumu chini ya mwavuli wa SAMIDRC kupoteza maisha.
Alisema:”Kufuatia kuzidi kwa mapigano katika eneo la Mashariki mwa DRC, tumepoteza wanajeshi 13 shupavu waliokuwa wakitimiza majukumu yao kwa uaminifu na kujitoa kwao kwa ajili ya amani. Mapigano haya ni matokeo ya kuongezeka kwa mashambulizi ya kundi la waasi la M23 na wanajeshi wa Rwanda Defence Force (RDF) dhidi ya FARDC na walinda amani wa SAMIDRC.”
Katika hotuba yake ambayo pia ameiweka kwenye mtandao wa X, Ramaphosa alisisitiza Serikali ya Afrika Kusini inatoa msaada wa kila hali kwa familia za waliopoteza maisha na kwamba taratibu za kuwarejesha nchini zinakamilishwa.
Aliendelea kusema: “Tunawaheshimu na kuwaomboleza” na kusisitiza kuwa Afrika Kusini haina nia ya kupigana vita dhidi ya taifa lolote, bali inaunga mkono juhudi za kuleta amani DRC kupitia SADC na Umoja wa Mataifa.
Alisema: “Uwepo wa wanajeshi wa Afrika Kusini katika Mashariki mwa DRC si tangazo la vita dhidi ya nchi yoyote, bali ni sehemu ya juhudi za SADC na Umoja wa Mataifa za kuleta amani na kulinda maelfu ya watu walioko hatarini.”
Ramaphosa pia aliunga mkono msimamo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ulioagiza kusitishwa kwa mapigano mara moja, kukomeshwa kwa upanuzi wa eneo linaloshikiliwa na M23, kuondoka kwa vikosi vya kigeni kutoka DRC na kurejeshwa kwa mazungumzo ya amani chini ya mchakato wa Nairobi.
Alihimiza kuheshimiwa kwa mipaka ya DRC na kueleza kuwa taifa hilo linapaswa kulindwa kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa kisiasa na mipaka ya mataifa.
Katika mkutano wa kilele wa dharura wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika jana Jumatano Januari 29, Rais Kagame alitoa matamshi makali dhidi ya Serikali ya DRC na washirika wake wa kijeshi. Alitilia mkazo dhuluma wanazokumbana nazo watu wa jamii ya Watutsi walioko DRC.
“Wamewahamisha watu, wamewaua watu, wamewatesa kila siku kwa sababu ya wao ni nani. Tuna wakimbizi walioko Rwanda kwa zaidi ya miaka ishirini, wakitengwa kutoka Congo na kulazimishwa kupelekwa Rwanda kwa madai kuwa wao ni Watutsi, hivyo basi wanapaswa kuwa Rwanda na si DRC,” alisema Kagame.
Kagame alieleza jamii ya kimataifa, pamoja na walinda amani wa Monusco na SAMIDRC, wamekuwa wakishuhudia hali hii kwa miaka mingi bila kuchukua hatua madhubuti.
Alihoji; “Tuna Monusco, tuna SAMIDRC, tuna mamluki, tuna Burundi, tuna FDLR waliojiunga nao na kila mtu yuko pale akitazama hali hii ikitokea, lakini tunajifanya hatuelewi kinachoendelea kwa miaka yote hii?”
“Kisha tunaposhuhudia matukio kama yale ya wiki iliyopita, tunajifanya kushangaa na kuzungumza kuhusu janga la kibinadamu. Je, si mateso haya ya kila siku, mauaji na uhamishaji wa watu si sehemu ya hali hiyo ya kibinadamu? Kama Afrika Mashariki, tunakaa hapa, lakini tunafanya nini kuhusu hali hii,” alihoji Kagame.
Katika kauli nyingine iliyoweka wazi mvutano wake na Afrika Kusini, Kagame alidai Ramaphosa anajifanya mpatanishi ilhali ana vikosi vinavyopigana upande wa serikali ya DRC dhidi ya M23.
“Kwa siku mbili zilizopita, Jumatatu na Jumanne, nilizungumza na Rais wa Afrika Kusini (Cyril Ramaphosa), aliyenitafuta ili kujadili ushiriki wake Mashariki mwa Congo. Anajifanya kuwa mpatanishi, ilhali ana jeshi lake likipigana bega kwa bega na M23 kwa maelekezo ya Rais Tshisekedi. Hawa ni watu ambao hawapaswi kuwa Congo. M23 si Wanyarwanda; ni Wakongo. Wakati mwingine anakiri hilo, lakini mara nyingine anakanusha,” alisema Kagame.
Kagame pia alionya mashambulizi yanayoelekezwa kwa raia wa Rwanda kutoka DRC hayawezi kuvumiliwa, akisisitiza Rwanda itajibu kwa nguvu ikiwa hali itaendelea.
“Siku chache zilizopita, tumepoteza watu wetu. Kulikuwa na mashambulizi makali kutoka Mashariki mwa Kongo, kutoka Goma, yaliyoangamiza maisha ya watu kadhaa na kuwajeruhi mamia. Tutalishughulikia jambo hili bila swali,” alionya.
Mvutano wa kidiplomasia na mustakabali wa mgogoro
Kauli kali kati ya Kagame na Ramaphosa zinaonyesha mgogoro wa DRC si tu changamoto ya ndani bali pia tatizo la kikanda linalogusa mataifa yenye nguvu barani Afrika.
Hali hii inaathiri uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa haya mawili, huku Afrika Kusini ikijitokeza wazi kama mshirika wa Serikali ya DRC, wakati Rwanda inaendelea kukanusha kuhusika moja kwa moja na uungaji mkono wa M23.
Mkutano wa EAC uliofanyika kwa dharura ulisisitiza wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja na kuanzishwa kwa mazungumzo ya amani, lakini kwa mtazamo wa sasa, suluhisho la mgogoro huu linaonekana kuwa gumu. Hali inavyoendelea, ni wazi kuwa msuguano kati ya viongozi hawa wawili utaendelea kuwa sehemu ya mjadala wa kisiasa na kijeshi barani Afrika.
Kwa kuzingatia hali hii, swali linabaki: Je, Afrika Mashariki itafanikiwa kupata suluhu ya kudumu, au mgogoro wa DRC utaendelea kuwa chanzo cha migogoro ya kisiasa na kijeshi katika ukanda huu?