Simiyu. Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Simiyu iliyopo mjini Bariadi, Latipha Juma (17) amejiua kwa kujinyonga kwa mtandio chumbani kwake, huku sababu za kufanya uamuzi huo zikiwa hazijafahamika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Januari 30, 2025 kwa waandishi wa habari na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe, tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Januari 30, 2025 katika Mtaa wa Kidinda mjini Bariadi.
Kamanda Swebe amesema Januari 29, 2025 saa 3 usiku, marehemu aliagana na mama yake mzazi, Happiness Lushiba kuwa anakwenda kulala ikiwa ni muda mfupi baada ya kumaliza kula chakula cha usiku.
Amesema kulipokucha, saa 1:00 asubuhi mama yake alikwenda kumuamsha ili aende shule lakini hakujibiwa, ndipo alipokwenda kuchungulia kupitia dirisha la chumba alichokuwa amelala, akamuona akining’inia juu ya kenchi.
Kamanda Swebe amesema jeshi hilo bado linachunguza chanzo cha tukio hilo, huku akitoa wito kwa wazazi kuwa na ukaribu na watoto wao ili kutambua changamoto wanazokutana nazo.
Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi mkoani humo limewakamata watu wawili; Emeli Opi na Mangu Kitula ambao ni viongozi wa Kijiji cha Mwabadimu kilichopo Wilaya ya Bariadi kwa kushirikiana na baadhi ya wanakijiji katika tukio la kuchoma moto nyumba 10 na kuharibu mali na mifugo pamoja na kukatakata mazao ya Ngusa Konya (50), mkazi wa kijiji hicho.
Tukio hilo limetokea Januari 21, 2025 saa 5:00 asubuhi katika Kitongoji cha Mwalula ambapo thamani halisi ya athari ya uharibifu huo bado haijapatikana na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na baada ya kukamilika washitakiwa watafikishwa mahakamani.
Kamanda Swebe amesema jeshi hilo linaendelea kuwasaka watu wote ambao kwa namna moja au nyingine wameshiriki katika tukio hilo la uharibifu wa nyumba hizo pamoja mali na mazao shambani.
Pia, ametoa rai kwa wananchi kuacha mara moja vitendo vya kujichukulia sheria mkononi.