Washington DC. Ndege ya abiria iliyokuwa ikitokea Wichita Mjini Kansas nchini Marekani imegongana na Helkopta ya Jeshi la nchi hiyo wakati ikitua kwenye Uwanja wa Reagan jijini Washington DC.
Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia leo Alhamisi Januari 30,2025 wakati ndege hiyo ya abiria ya Shirika la American Airlines yenye namba za usajili 5342 iliyokuwa ikitua uwanjani hapo.
Ndege hiyo ilikuwa na abiria 60 na wahudumu wanne wakati helkopta ya kijeshi ikiwa na wanajeshi watatu.
Taarifa zinaeleza kuwa tayari Mamlaka ya Usimamizi wa Anga na Ulinzi nchini Marekani, zimepeleka kikosi cha uokoaji uwanjani hapo. Hata hivyo, taarifa za awali zinadai kuwa hakuna madhara yaliyothibitishwa kwa binadamu.
“Watumishi wa Idara ya dharura wameshafika eneo la ajali ya ndege hizo ilipotokea. Uwanja unaendelea kuwa wazi japo safari zimesimamishwa kwa muda,” imesema taarifa ya mamlaka ya usimamizi wa uwanja wa Reagan iliyochapishwa kwenye ukurasa wa X (zamani Twitter).
Tayari Rais wa Marekani, Donald Trump ameshajulishwa kuhusu ajali hiyo huku Makamu wake, JD Vance akiandika kwenye akaunti yake ya X kuwa: “Tumuombee kila mmoja aliyekuwemo kwenye ndege hizo.”