NYOTA watatu wa ‘Nyuki wa Tabora’ Tabora United, waliokuwa wanahofiwa kukosa mchezo wa Jumapili hii ya Februari 2, dhidi ya Simba, wamekamilisha taratibu zote hivyo kwa sasa wako tayari kwa ajili ya kukipambania kikosi hicho cha mkoani Tabora.
Wachezaji hao ni kipa, Jean-Noel Amonome aliyetokea AS Arta/Solar7 ya Djibouti, winga Joseph Akandwanaho aliyetoka Mbarara City FC ya kwao Uganda na kiungo mkabaji raia wa Cameroon, Martial Zemba Ikoung kutokea Union Touarga Sportif.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Tabora United, Adam Simba alisema taratibu zote za vibali kwa wachezaji hao zimekamilika hivyo mashabiki zao wawe na imani kubwa ya kuwaona uwanjani wakicheza kuanzia mchezo wao dhidi ya Simba.
“Tulishakamilisha taratibu zote kwa ajili ya wachezaji wetu ambao walikuwa na shaka ya kucheza dhidi ya Simba Jumapili hii, kilichobaki ni kwa benchi la ufundi kuamua wenyewe kuwatumia au kutowatumia kutokana na mahitaji yao,” alisema.
Mbali na nyota hao wa kigeni waliojiunga na timu hiyo katika dirisha dogo, wengine ni kipa Fikirini Bakari aliyetokea Fountain Gate, beki wa kati, Yassin Mustapha aliyesajiliwa akiwa huru na mshambuliaji, Emmanuel Mwanengo kutoka FK Vakhsh Bokhtar ya Tajikistani.
Mchezo huo ni wa kisasi wa wenyeji ambao mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Mwenge jijini Dar es Salaam, Agosti 18, mwaka jana, Simba ilishinda mabao 3-0, yaliyofungwa na Che Malone Fondoh, Valentino Mashaka na Awesu Awesu.