Kigali. Mzozo kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na waasi wa M23 umechukua sura mpya baada ya Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa kuishutumu Rwanda kuwa inawafadhiri waasi wa M23 ambao anadai waliwaua wanajeshi 13 wa Afrika Kusini.
Kufuatia vifo hivyo, Serikali ya Afrika Kusini ilitoa taarifa kupitia mtandao wake wa kijamii wa X (zamani Twitter), ikitoa salamu za pole kwa familia za waliopoteza maisha na kuishutumu Rwanda kwa kushirikiana na waasi wa M23 katika mashambulizi hayo.
Taarifa ya Serikali ya Afrika Kusini kwa Umma imeandikwa: “Wapendwa wananchi wa Afrika Kusini, kutokana na kuongezeka kwa mapigano mashariki mwa DRC, tumepoteza wanajeshi wetu 13 shujaa waliokuwa wakipigania amani.
“Mapigano haya yamechochewa na waasi wa M23 kwa kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) dhidi ya vikosi vya FARDC na walinda amani wa Misheni ya SADC (SAMIDRC).
“Kwa niaba ya serikali na wananchi wa Afrika Kusini, tunatoa pole kwa familia za waliopoteza maisha na tunawaenzi kwa ujasiri wao. Msaada wote muhimu unapatikana kwa familia zilizoathirika huku taratibu za kuwarejesha nyumbani waliofariki zikiendelea.
“Mashambulizi haya yameathiri pia wanajeshi kutoka Malawi, Tanzania na wanachama wa MONUSCO. Hali katika miji ya Goma na Sake bado ni tete na isiyotabirika, lakini juhudi zinaendelea kuhakikisha vikosi vya SAMIDRC vinapokea msaada wa kutosha.”
“Uwepo wa wanajeshi wetu mashariki mwa DRC haupaswi kutafsiriwa kama tangazo la vita dhidi ya taifa lolote, bali ni juhudi za kuleta amani chini ya Umoja wa Mataifa na SADC. Tunasisitiza pande zote kushiriki juhudi za kidiplomasia ili kupata suluhisho la kudumu.”
Jana, viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) waliitisha mkutano wa dharura kujadili suala hilo, hata hivyo Rais wa DRC, Felix Tshisekedi hakuhudhuria.
Shirika la Habari la Reuters limeripoti kuwa hasimu wake, Rais wa Rwanda, Paul Kagame alishiriki mkutano huo na kuahidi kushiriki katika jitihada za kuleta amani mashariki mwa DRC japo alikana kuhusika kuwafadhili M23.
Mkutano wa dharura EAC, yenye wanachama wanane, uliazimia kuwa mapigano hayo yasitishwe na kuitaka Serikali ya DRC kukutana na uongozi wa M23 kwa ajili ya kufikia makubaliano ya pande zote ya kusitisha mapigano hayo.
Hata hivyo, Tshisekedi akihutubia Umma wa DRC kwa wakati tofauti kuhusiana na uvamizi huo wa M23 jana alisema: “Uwepo wa maelfu ya wanajeshi wa Rwanda katika ardhi yetu….unachochea vita na madhara zaidi.”
Uamuzi wa mkutano huo wa EAC unaoana na kauli ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lililotaka kusitishwa kwa mapigano hayo baada ya waasi wa M23 kuanza uvamizi na kuuteka mji wa Goma.
Rais Kagame alikanusha tuhuma hizo, akizitaja kuwa za uongo na kinyume na mazungumzo aliyokuwa nayo na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa na kumtaja kuwa amepotosha mazungumzo yao ya faragha waliyofanya na kusema kama Afrika Kusini inataka makabiliano basi Rwanda iko tayari kujibu.
Katika waraka wake mzito alioandika kwenye Mtandao wake wa X, Rais Kagame amesema alifanya mazungumzo mawili wiki hii hususan jana na Rais Ramaphosa kuhusu hali ya Mashariki mwa DRC, akisema kuwa kile kilichosemwa na maofisa wa Afrika Kusini na Rais Ramaphosa mwenyewe kuhusu mazungumzo yao kwenye vyombo vya habari kimejaa upotoshaji mwingi.
Rais Kagame amesema ikiwa maneno yanaweza kubadilika kiasi hicho kutoka kwenye mazungumzo hadi kwenye tamko la umma, inasema mengi kuhusu namna masuala haya muhimu yanavyoshughulikiwa.
Rais Kagame amesema ikiwa Afrika Kusini inataka kuchangia suluhisho la amani huko Mashariki mwa DRC hilo ni jambo jema, lakini haina nafasi ya kuchukua jukumu la mpatanishi au msuluhishi. Na iwapo Afrika Kusini itataka makabiliano, Rwanda iko tayari kujibu.
Kagame alidai Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) si kikundi cha waasi bali ni jeshi rasmi la Rwanda, akidai kuwa misheni ya SADC nchini DRC (SAMIDRC) inalenga kushambulia wananchi wa DRC na kuivamia Rwanda kijeshi.
Rais Kagame alijibu madai ya Afrika Kusini kwamba vikosi vyake vinahusika kwa kuandika:
“Nimefanya mazungumzo na Rais Ramaphosa kuhusu hali mashariki mwa DRC, lakini taarifa zinazotolewa na maofisa wa Afrika Kusini ni za upotoshaji badala yake Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) ni jeshi rasmi, si kikundi cha waasi.
“Pia, SAMIDRC si kikosi cha ulinzi wa amani bali ni jeshi la mashambulizi lililotumwa kusaidia serikali ya DRC kupigana dhidi ya raia wake, likishirikiana na vikundi vya kigaidi kama FDLR ambavyo vinatishia usalama wa Rwanda.
“SAMIDRC ilihusika na kuondolewa kwa Vikosi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki, jambo ambalo limehujumu juhudi za mazungumzo ya amani.
“Rais Ramaphosa hakutoa onyo lolote dhidi ya Rwanda, bali aliomba msaada wa chakula, maji, na umeme kwa wanajeshi wake.
“Wanajeshi wa Afrika Kusini hawakuuawa na M23, bali waliuawa na vikosi vya FARDC.
“Ikiwa Afrika Kusini inataka kusaidia amani, tunakaribisha juhudi hizo. Lakini kama wanataka mzozo, Rwanda iko tayari kukabiliana nao,” Amesema Kagame.
Mzozo kati ya Afrika Kusini na Rwanda unaendelea kuwa na mvutano mkubwa huku pande zote zikitupiana lawama kuhusu mapigano yanayoendelea mashariki mwa DRC.
Ingawa juhudi za kidiplomasia zinahitajika, mvutano huu unaonyesha ugumu wa kuleta amani katika eneo hilo lenye migogoro ya muda mrefu.
Vita hiyo iliyoanza kufukuta siku nne zilizopita kwa waasi wa M23 kuyateka maeneo ya Mashariki mwa DRC ukiwemo Mji wa Goma.
Jana, pia, zilisambaa video za mamluki maarufu kama ‘Mercenaries’ ambao ni askari wa kukodi zaidi ya 200 kutoka mataifa ya Ulaya, wengi wao kutoka nchini Romania ambao walisalimu amri kwa waasi ya M23 kisha waasi hao kuwaruhusu kuingia nchini Rwanda ambako waliruhusiwa kurejea nchini kwao.
Katika mazungumzo na Reuters, mmoja wa mamluki hao (hakutaja jina) alisema walipelekwa nchini DRC kwa lengo la kuwafundisha wanajeshi wa Jeshi la DRC, FARDC mbinu za kivita na matumizi ya silaha. Hata hivyo alieleza kujifunza kuwa nyakati hubadilika muda wowote.
Reuters pia imeripoti kuwa wakati jitihada za kukomesha mapigano hayo zikiendelea, waasi wa M23 wameendelea kusonga mbele na sasa wameusogelea Mji wa Bukavu ulioko Jimbo la Kivu Kusini nchini humo.