Kwa mujibu wa ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) ya kipindi cha robo mwaka kilichoishia Desemba, 2024, idadi ya laini za simu iliongezeka kutoka 70,290,876 mwaka 2023 hadi kufikia 86,847,460 mwaka 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 23.5.
Kwa upande wa watumiaji wa huduma za miamala, idadi ya akaunti iliongezeka kutoka 52,875,129 hadi kufikia 61,882,499 sawa na ongezeko la asilimia 17, hata hivyo, ongezeko hilo halikuleta athari chanya katika kipengele cha idadi ya miamala.
Ripoti hiyo iliyotolewa mapema mwezi huu inaonyesha kupungua kwa idadi ya miamala kutoka 5,273,086,154 mwaka 2023 hadi kufikia 3,737,202,434 mwaka 2024, ikiwa ni sawa na pungufu ya asilimia 29.
Kutokana na anguko hilo la idadi ya miamala, Profesa Dickson Pastory, ambaye ni mchambuzi wa uchumi, anasema kuwa ongezeko la kodi na tozo kwenye miamala ni miongoni mwa sababu kuu zinazowafanya watumiaji kutafuta njia mbadala za kutekeleza miamala yao. “Kwa sababu ya tozo kubwa, watu wanageukia huduma nyingine kama za kibenki, ambazo kwa sasa zinaonekana kuwa nafuu zaidi,” anasema Profesa Pastory, ambaye ni mhadhiri katika Chuo cha Biashara (CBE).
Profesa Pastory anasema mbali na sababu hizo alizozieleza, kikwazo kingine ni hali duni ya kiuchumi kwa watu wengi. “Mwaka 2024, mifuko ya watu haikuwa imara sana, hali iliyowafanya kushindwa kufanya miamala kwa wingi.”
Kwa upande wake, Mhadhiri mwandamizi kutoka Shule Kuu ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Thobias Swai, alisema kuwa uelewa wa watu kuhusu gharama za tozo na kodi umesababisha mabadiliko katika tabia za kifedha.
Swai anasema jambo hilo limewafanya wengi kuchagua kufanya miamala michache lakini ya thamani kubwa ili kupunguza gharama za tozo. “Kutokana na kuongezeka kwa gharama za tozo na kodi, watu wameamua kuunganisha miamala yao ili iwe mikubwa lakini michache, badala ya kufanya miamala midogomidogo mara nyingi,” alisema Dk Swai.
Dk Swai, ambaye ni mbobezi wa masuala ya fedha alielezea kuwa sababu nyingine ni mabadiliko ya kiteknolojia na urahisishaji wa miamala ya kifedha kati ya benki yamekuwa sababu nyingine ya kupungua kwa matumizi ya huduma za kifedha kupitia simu za mkononi.
“Uzinduzi wa TIPS (Tanzania InterBank Payment System) mnamo Machi 2024 umevutia watumiaji wengi kwa sababu ni njia nafuu, ya haraka, na rahisi kutuma fedha moja kwa moja kutoka benki moja kwenda nyingine,” anaeleza Dk Swai.
Aliongeza kuwa mfumo huo mpya umekuwa mwarobaini kwa changamoto zilizokuwepo awali za urasimu na gharama kubwa katika uhamishaji wa fedha kupitia benki, hivyo kuzidi kuvutia wateja wengi kuhamia kwenye huduma za kibenki badala ya huduma za simu za mkononi.
Aidha, Profesa Anna Sikira ambaye ni mchumi kutoka chuo kikuu cha SUA, anakubaliana na wanazuoni wenzake kuhusu athari za gharama kubwa za utumaji pesa, akibainisha kuwa hali hiyo inawalazimisha watu kutafuta njia mbadala za kufanya miamala yao.
“Unakuta mtu anatuma fedha kidogo, lakini makato yanakuwa makubwa. Mtumiaji anaona hailipi, hivyo anachagua kutafuta njia nyingine za kiuchumi zaidi,” anasema Profesa Sikira.
Pia anaongeza kuwa ingawa mitandao ya kifedha inaendelea kunufaika kutokana na makato haya, mzigo mkubwa unabebwa na mtumiaji wa mwisho.
“Ni kweli kwamba watoa huduma za kifedha wanakabiliana na gharama kubwa za ada zinazotozwa, lakini ukilinganisha tozo hizi na gharama wanazopata wao, ni wazi kwamba mtumiaji wa huduma ndiye anayepata madhara zaidi,” anafafanua Profesa Sikira.
Anasisitiza kuwa ili kurejesha imani ya watumiaji na kuongeza matumizi ya huduma za kifedha, kunahitajika mabadiliko ya sera zinazohusiana na kodi na tozo ili kuhakikisha mizani ya gharama inakuwa ya haki kwa pande zote.
Aidha, licha ya ongezeko la bei ya huduma ya data kutoka Sh1.73 kwa megabaiti moja (1 MB) mwaka 2020 hadi Sh2.17 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 25, idadi ya laini za simu zinazotumia huduma hiyo ya mtandao imeongezeka kwa kasi kubwa.
Takwimu zinaonyesha kuwa laini hizo ziliongezeka kutoka 26,078,506 mwaka 2020 hadi kufikia 48,028,227 mwaka 2024, ongezeko la asilimia 84.
Ongezeko hili linaonyesha jinsi teknolojia ya mtandao ilivyoingia katika maisha ya kila siku, ikiimarisha mawasiliano, biashara, na burudani kwa watu wengi.
Mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, TikTok, na X (zamani Twitter) imekuwa kivutio kikubwa kwa watumiaji wa data, hasa vijana, ambao hutumia majukwaa haya kwa madhumuni mbalimbali.
“Ninapenda kutumia TikTok, Youtube, Whatsapp pamoja na Instagram kwa sababu zinatoa burudani ya haraka na ya kufurahisha. Pia, nazitumia zaidi katika masomo yangu chuoni. Hivyo nalazimika kununua bando pasipo kuangalia bei yake,” alisema Mariam Ahmed, mwanafunzi wa Chuo cha Uandishi, Morogoro. Ukuaji huu mkubwa wa matumizi ya mtandao umechangiwa pia na juhudi za watoa huduma za simu kuboresha upatikanaji wa mtandao wa kasi zaidi kama vile 4G na 5G, na kuongeza maeneo ya kufikiwa na huduma hizo.
Takwimu zinaonesha kuwa asilimia ya watu waliofikiwa na huduma ya 4G ni 88, huku wale waliofikiwa na 5G wakiwa 20%. Vilevile, asilimia ya maeneo yaliyo na mawasiliano ya 4G ni 71, wakati huduma ya 5G imefikia maeneo 2.5% pekee.
Pia, uwepo wa simu za bei nafuu zinazounga mtandao umechangia kuwawezesha watu wa kipato cha chini kuingia kwenye ulimwengu wa kidijitali.