Sheikh Muhammad Idd afariki dunia, kuzikwa kesho Tanga

Sheikh maarufu nchini Sheikh Muhammad Idd Muhammad, amefariki dunia leo tarehe 30, Januari, 2025
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, kifo chake kimetokea katika Hospitali ya Mloganzila alikokuwa akipatiwa matibabu.

Hadi mauti yanamfika, Sheikh huyu maarufu pia kwa jina la Abu Idd alikuwa mshauri wa Mufti kwenye masuala ya jamii na Imam wa Msikiti wa Mnyamani uliopo Buguruni jijini Dar es Salaam.
Aidha, Sheikh Abu Idd alikuwa pia Katibu wa Jopo la Masheikh na Wanazuoni wa Kiislam Tanzania.

Taratibu za mazishi zinaendelea na mwili unatarajiwa kuzikwa kesho Januari 31, 2025 kijijini kwake Kata ya Mkata, Handeni mkoani Tanga.

Taarifa ya mazishi inaonyesha kuwa mwili wake utaoshwa na kuswaliwa katika Msikiti wa Mnyamani uliopo Buguruni  leo wakati wa swala ya Adhuhuri, sambamba na visomo vitakavyofanyika msikitini hapo.

Taarifa imeongeza baadaye alasiri,  mwili wake utapelekwa makao makuu ya Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) na kuswaliwa tena kabla ya kusafirishwa kuelekea Mkata kwa maziko yatakayofanyika baada ya Swala ya Ijumaa.

Endelea kufuatilia katika mitandao ya Mwananchi

Related Posts