Takukuru wambana kiongozi wa Vicoba aliyedaiwa kukwapua Sh13 milioni

Rombo. Taasisi Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, imefanikiwa kurejesha zaidi ya Sh13.7 milioni za kikundi cha benki za jamii (Vicoba) cha Samaria, kilichopo Kijiji cha Holili Vjijini.

Imedaiwa kuwa fedha hizo zilichukuliwa na mmoja wa viongozi wa kikundi hicho (jina limehifadhiwa), baada ya kutokomea kusikojulikana na hivyo ndugu zake wamebanwa na kuzilipa.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Januari 30, 2025 na Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Mussa Chaulo alipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa.

“Takukuru tumefanikiwa kurejesha kiasi cha Sh 13.7 milioni iliyofanyiwa ubadhirifu na makamu mwenyekiti wa kikundi cha kusaidiana cha Samaria, (amemtaja jina).

“Baada ya Takukuru kuanza kumtafuta ndugu wa kiongozi huyo aliwatafuta wananchama wanaodai fedha zao na kurejesha fedha hizo kwa awamu, hadi Desemba 28, 2024 fedha hizo zote kiasi cha Sh 13.7 milioni zilikuwa zimerejeshwa kwa wanachama hao,” amesema Chaulo.

Katika hatua nyingine, Takukuru imefanya ufutatiliaji wa fedha za umma katika miradi 26 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh11 bilioni katika sekta ya afya, elimu, maji na ujenzi wa barabara na kubaini mapufungu katika sekta ya afya na elimu yenye thamani ya Sh3.7 bilioni.

“Tumefanya ufuatiliaji wa fedha za umma katika miradi ya maendeleo kwenye Wilaya Saba za Mkoa wa Kilimanjaro, kwenye miradi 26 yenye thamani ya Sh11 bilioni katika sekta za afya, elimu, maji na ujenzi wa barabara, miradi iliyobainika kuwa na mapungufu ni  katika sekta ya afya na elimu,” amesema.

Amesema miradi iliyobainika kuwa na upungufu  katika sekta ya afya na elimu ambayo thamani yake ni Sh3.7 bilioni, kasoro zimebainika upande wa milango na samani kutokuwa na ubora huku akisema aliyepewa kazi ya kujenga shule imebainika hakuwa na uwezo wa kutekeleza miradi aliyopewa.

Related Posts