Mbeya. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Mbeya limeiomba Halmashauri ya Jiji la Mbeya kushirikiana nalo kubaini mtandao wa wahalifu wanaojihusisha na wizi wa nyaya za mifumo ya transfoma, ambao umeongezeka.
Kwa mujibu wa Ofisa Uhusiano wa Huduma kwa Wateja wa Tanesco Mbeya, Christina Shoki, kati ya Novemba Mosi, 2024 na Januari 3, 2025, jumla ya transfoma 36 zimehujumiwa na wahalifu wasiojulikana.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani la Jiji la Mbeya leo Alhamisi, Januari 30, 2025, Shoki amesema kuna ongezeko kubwa la uharibifu wa miundombinu ya shirika, hasa nyaya za shaba (copper), ambazo ni kiungo muhimu katika mfumo wa usambazaji wa umeme bora kwa wananchi.
“Kutokana na hali hii, Tanesco kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi limeendesha msako na kufanikiwa kuwakamata baadhi ya watuhumiwa wakiwa na vifaa mbalimbali, zikiwemo nyaya za shaba zinazotumika kwenye transfoma,” amesema Shoki.
Amesisitiza kuwa ili kukomesha uhalifu huu, Tanesco inaomba ushirikiano wa Baraza la Madiwani katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari za vitendo hivi na kusaidia kubaini wahusika pamoja na masoko ya vifaa vinavyoibiwa.
“Tunaomba kupitia baraza hili, madiwani mtusaidie kuwaelimisha wananchi kuhusu madhara ya kuhujumu miundombinu ya umeme kupitia mikutano ya hadhara ili kufanikisha jitihada za kudhibiti wizi huu,” amesema Shoki.
Amesema uchunguzi wa shirika umebaini nyaya za shaba ndizo zinazoibwa zaidi, hali inayosababisha hasara kubwa na kuathiri upatikanaji wa huduma ya umeme.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa amewataka madiwani kusimamia vyema utekelezaji wa miradi iliyopangwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati.
“Madiwani, kupitia rasimu yetu ya bajeti, tunatarajia miradi yote iliyobaki itakamilika kwa wakati, na fedha zitatolewa kwa kila kata kati ya 36 zilizopo,” amesema Issa.
Aidha, amesema Halmashauri ya Jiji kwa kushirikiana na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson, imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa lengo la kuifanya Mbeya kuwa jiji la kisasa zaidi.
Naye Diwani wa Kata ya Maendeleo, Issa Salimin, alishauri Tanesco kufanya mikutano ya hadhara katika kila kata ili kuwaelimisha wananchi kuhusu sababu za kukatika kwa umeme na athari za wizi wa miundombinu hiyo.
“Tunaona mara kwa mara umeme unakatika bila taarifa rasmi. Ni vyema Tanesco wakatoa elimu kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara ili kueleza sababu na kuhamasisha ushirikiano wa kukomesha uhalifu huu,” amesema Salimin.
Mkazi wa Kata ya Mabatini, Tausi Joel amesema ni vema Tanesco ikaanzisha mfumo wa ulinzi shirikishi utakaohusisha wananchi kwa karibu zaidi.
“Wahalifu hawa ni miongoni mwetu, tunajuana. Tanesco inapaswa kujenga mahusiano mazuri na jamii ili watu waweze kutoa taarifa kwa siri kuhusu mtandao wa wahalifu na masoko ya vifaa vinavyoibwa,” amesema Tausi.