Dar es Salaam. Saa chache tangu ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa kikodi Kariakoo kuwaka moto, mamlaka hiyo imezihamishia kwa muda huduma zake katika majengo ya Diamond Plaza na Mariam Tower.
Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi Januari 30, 2025 na idara ya elimu kwa mlipakodi ya mamlaka hiyo.
“Kufuatia janga la moto lililotokea leo Januari 30, 2025 katika ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Kikodi Kariakoo iliopo Mtaa wa Kipata, tunapenda kuwafahamisha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kwamba, huduma zote zimehamishiwa kwa muda katika ofisi zetu zilizopo jengo la Diamond Plaza, lililopo makutano ya barabara ya Samora na mtaa wa Mirambo, Kata ya Kivukoni, pamoja na ofisi ya TRA iliyopo jengo la Mariam Tower, mtaa wa Shauri Moyo, eneo la Shule ya Uhuru jijini Dar es Salaam,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: “Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inapenda kuwashukuru Jeshi la Polisi, pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, na wananchi wote kwa ujumla kwa jitihada kubwa walizoonesha kufanikisha udhibiti wa janga la moto lililojitokeza.”